Michezo

AFCON: Rohr amemsifu kinda baada ya Nigeria kufanikiwa kupiga Burundi

June 24th, 2019 1 min read

JOHN ASHIHUNDU

CAIRO, Misri

Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria, Gernot Rohr amemsifu kinda Ola Aina kutokana mchango wake mkubwa walipokabiliana na Burundi katika pambano lao la ufunguzi la AFCON, mwishoni mwa wiki.

Rohr alimsifu mlinzi huyo matata wa klabu ya Torino ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kuchezea Super Eagles ambayo iliibuka na ushindi wa 1-0.

Aina alichangia kuingia kwa bao hilo la Odion Ighalo ambaye alifunga kwa kutumia kizigino zikisalia dakika 13 mechi hiyo kumalizika.

Rohr alisema kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 amebarikiwa kipaji cha kucheza kama beki wa pembeni na pia kama mshambuliaji wa pembeni

”Ola Aina ameimarika zaidi. Alijifunza kucheza katika safu tufuati alipokuwa katika kituo cha kunoa vipawa cha Chelsea,” Rohr aliwaambia waandishi baada ya ushindi huo.

”Ni mchezaji muhimu kikosini kwa sababu anweza kutegemewa katika safu zote, kuanzia nyuma hadi safu ya ushambuliaji.”

Aina ambaye ni mzaliwa na London, aliichezea Nigeria kwa mara ya kwanza mnamo 2017 katika mechi ya mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.