AFCON: Salah abeba Misri dhidi ya Guinea-Bissau katika Kundi D

AFCON: Salah abeba Misri dhidi ya Guinea-Bissau katika Kundi D

Na MASHIRIKA

MOHAMED Salah alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Misri dhidi ya Guinea-Bissau katika mchuano wa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Jumamosi nchini Cameroon.

Hata hivyo, mabingwa hao mara saba wa AFCON waliponea chupuchupu baada ya refa aliyerejelea teknolojia ya VAR kufutilia mbali bao la Mama Balde wa Guinea-Bissau mwishoni mwa kipindi cha pili.

Misri walijibwaga ugani wakiwa na ulazima wa kushinda mechi hiyo baada ya kupigwa 1-0 na Nigeria katika pambano la ufunguzi wa Kundi D.

Miamba hao walianza mechi kwa matao ya juu na wakashuhudia makombora yao matatu yakigonga mwamba wa lango la Guinea-Bissau kabla ya Salah wa Liverpool kucheka na nyavu katika dakika ya 21 na kumwacha hoi kipa Jonas Mendes mjini Garoua.

Misri kwa sasa wanakamata nafasi ya pili kwenye Kundi D kwa alama tatu nyuma ya viongozi Nigeria waliopepeta Sudan 3-1 katika mchuano mwingine wa kundi hilo mnamo Jumamosi usiku.

Misri watatamatisha kampeni zao za makundi dhidi ya Sudan mnamo Januari 19, 2022 wakifahamu kwamba sare ya aina yoyote itawakatia tiketi ya hatua ya 16-bora.

Guinea-Bissau kwa upande wao watakuwa na ulazima wa kuangusha Nigeria ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa raundi hiyo ya muondoano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WALIOBOBEA: Kosgey; Waziri msiri na mwaminifu kwa Kibaki

Luis Nani ajiunga na klabu ya Venezia

T L