AFCON: Tunisia waponda Mauritania bila huruma katika Kundi F

AFCON: Tunisia waponda Mauritania bila huruma katika Kundi F

Na MASHIRIKA

TUNISIA walijinyanyua katika Kundi F kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Cameroon kwa kutandika Mauritania 4-0.

Mabingwa hao wa AFCON 2004 walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Hamza Mathlouthi katika dakika ya nne kabla ya Wahbi Khazri kupachika wavuni goli la pili dakika nne baadaye. Khazri alicheka na nyavu kwa mara ya pili katika dakika ya 64 kabla ya Seifeddine Jaziri kuzamisha kabisa chombo cha Mauritania kunako dakika ya 66.

Tunisia walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kushinda ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele baada ya Mali kuwapokeza kichapo cha 1-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi F.

Youssef Msakni alitokea benchi katika kipindi cha pili na kunogesha makala ya saba ya fainali za AFCON. Hata hivyo, alipoteza penalti mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya mkwaju wake kupanguliwa.

The Carthage Eagles ya Tunisia ndicho kikosi cha pili baada ya wenyeji Cameroon kufunga mabao manne kufikia sasa kwenye fainali za AFCON mwaka huu. Sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu, moja pekee nyuma ya Gambia na Mali walioambulia sare ya 1-1 katika mchuano wao wa pili wa Kundi F.

Tunisia sasa watavaana na Gambia katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi F mnamo Januari 21, 2022. Mauritania ambao tayari wamepoteza mechi mbili kundini tayari wameaga kipute cha AFCON mwaka huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Everton waomba Ubelgiji wamruhusu Roberto Martinez awe...

Afueni kwa wakulima wa mashamba madogo bima ya mimea ya bei...

T L