AFCON: Wanane waaga dunia baada ya mkanyagano wa mashabiki kabla ya Cameroon kuvaana na Comoros

AFCON: Wanane waaga dunia baada ya mkanyagano wa mashabiki kabla ya Cameroon kuvaana na Comoros

Na MASHIRIKA

WATU wanane wameripotiwa kuaga dunia na wengi kuumia baada ya mashabiki kusukumana na kukanyagana nje ya uwanja wa Paul Biya kabla ya mechi ya hatua ya 16-bora kukutanisha wenyeji Cameroon na Comoros mnamo Jumatatu usiku.

Video zilionyesha maelfu ya mashabiki wakijitahidi kuingia uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo iliyochezewa viungani mwa jiji la Yaounde.

Kwa mujibu wa AFP, mtoto mmoja ni miongoni mwa mashabiki waliofariki huku baadhi wakipoteza fahamu.

Uwanja wa Paul Biya una uwezo wa kubeba mashabiki 60,000. Lakini kwa sababu ya kanuni za kudhibiti msambao wa virusi vya corona, uga huo haukustahili kubeba zaidi ya asilimia 80 ya mashabiki.

Kwa mujibu wa maafisa waliosimamia mechi hiyo, zaidi ya mashabiki 50,000 tayari walikuwa uwanjani kabla ya mkanyagano kushuhudiwa nje ya uwanja.

Katika taarifa yao, vinara wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) wamesema wameanzisha kuchunguza kisa hicho. Licha ya tukio hilo, mechi kati ya Cameroon na Comoros iliendelea na wenyeji wakashinda 2-1. Ushindi huo uliwakatia tiketi ya kuvaana na Gambia katika raundi ya robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

‘Kenya ingali inakabiliwa na changamoto za kuwapata...

Obiri atupia jicho mbio za mita 5000 baada ya kutamba...

T L