Michezo

#AFCON2019: Mataifa 14 yafuzu

November 19th, 2018 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUKU Kenya ikiendelea kusubiri uamuzi wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kufahamu kama imefuzu kushiriki Kombe la Afrika kwa wanaume wasiozidi umri wa miaka 23, mataifa 14 yameshajikatia tiketi.

Mataifa hayo ni Senegal na Madagascar (Kundi A), Morocco na Cameroon (Kundi B), Mali (Kundi C), Algeria (Kundi D), Nigeria (Kundi E), Guinea na Ivory Coast (Kundi H), Mauritania (Kundi I), Tunisia na Misri (Kundi J) na Uganda (Kundi L).

Makundi G na K yangali wazi, ingawa mabingwa wa Afrika mwaka 2012 Zambia wamebanduliwa nje baada ya kupoteza mechi ya tatu kwa kulimwa 1-0 na Msumbiji katika mechi za raundi ya tano Novemba 18. Kuna makundi 12. Kila kundi linatoa timu mbili.

Mechi kati ya Burundi na Gabon hapo Machi 22 mwaka 2019 nchini Burundi itakuwa kama fainali kwa sababu mshindi atajiunga na Mali katika AFCON kutoka Kundi C.

Sare itatosha kuweka Burundi katika kombe hili kwa mara yake ya kwanza kabisa. Gabon lazima ishinde Burundi ndiposa ishiriki AFCON kwa mara ya tatu mfululizo na nane kwa jumla. Mataifa ya Benin, Togo na Gambia bado yanasalia mbioni kuungana na Algeria kutoka Kundi D.

Hata hivyo, Benin iko katika nafasi nzuri zaidi kwa sababu imezoa alama saba, huku Togo na Gambia zikiwa alama mbili nyuma. Mechi kati ya majirani Benin na Togo hapo Machi mwaka ujao itakuwa kama fainali kwa sababu mshindi atajikatia tiketi. Gambia itafuzu ikiwa Benin na Togo zitatoka sare nayo ilemee Algeria.

Kundi E pia litawaka moto wakati wa mechi kati ya Libya na Afrika Kusini ambayo mshindi ataungana na Nigeria katika AFCON. Afrika Kusini ina alama tisa nayo Libya imezoa saba. Bafana Bafana inahitaji sare kutoka mchuano huu kujihakikishia nafasi katika makala yajayo.

Hatma ya Kundi F itaamuliwa na CAF kwa sababu kufikia sasa haijulikani kama Sierra Leone iko mashindanoni ama nje. Sierra Leone inatumikia marufuku ya muda usiojulikana kutoka kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya serikali kuingilia shughuli za shirikisho la soka nchini humo kwa madai ya ufisadi.

Kenya, Ghana, Ethiopia na Sierra Leone zinafuatana katika kundi hili kwa alama saba, sita, nne na tatu, mtawalia. Harambee Stars ya Kenya na Black Stars ya Ghana zitafuzu bila ya kupiga mpira Sierra Leone ikiondolewa. CAF inatarajiwa kutoa tangazo kuhusu hali ya kundi hili wakati wowote.

Kwa sasa, Kenya na Ghana zitalazimika kusuburi uamuzi huo. Kundi G linalojumuisha Zimbabwe (alama nane), Liberia (saba), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (sita) na Congo Brazzaville (tano) litamuliwa uwanjani Machi mwaka ujao. Bado liko wazi. Zimbabwe ilitupa nafasi murwa ya kufuzu Novemba 18 ilipobwagwa 1-0 nchini Liberia.

Congo ilikaba DR Congo 1-1 jijini Brazzaville. Zimbabwe itahitaji tu sare dhidi ya Congo kusonga mbele. Vita vya kujiunga na Mauritania kutoka Kundi I ni kati ya Angola na Burkina Faso ambazo zimezoa alama tisa na saba, mtawalia.

Angola iko pazuri zaidi kwa sababu itakamilisha ratiba dhidi ya wanyonge Botswana inayovuta mkia, bila ushindi. Burkina Faso inakodolea macho kukosa AFCON. Ilishiriki makala matano mfululizo yaliyopita. Itafuzu tu ikiwa Angola itapoteza dhidi ya Botswana nayo ichape Mauritania.

Guinea-Bissau, Namibia na Msumbiji zinang’ang’ania tiketi mbili kutoka Kundi K. Zote tatu zina nafasi ya kuwa katika AFCON 2019. Guinea-Bissau na Namibia zimevuna alama nane nayo Msumbiji iko alama moja nyuma. Guinea-Bissau itaalika Msumbiji nayo Namibia izuru Zambia katika mechi za raundi ya mwisho Machi mwaka 2019.

Chipolopolo ya Zambia, ambayo ilishiriki makala sita ya AFCON yaliyopita, haitakuwa nchini Cameroon kwa makala yajayo. Inavuta mkia katika kundi hili kwa alama nne.

Lesotho na Tanzania ziko bega kwa bega kwa alama tano kila mmoja katika Kundi L na katika vita vya kuwania tiketi moja iliyosalia katika kundi hili baada ya Uganda kufuzu moja kwa moja kama washindi wa kundi hili. Tanzania ingefuzu Novemba 18, lakini ikalemewa 1-0 nchini Lesotho.

Watanzania watakutana na Waganda katika mechi yao ya mwisho nayo Lesotho itazuru Cape Verde, ambayo imeshaaga mbio za kufuzu. Makala yajayo ya AFCON yatakuwa ya 32.

Tofauti na makala yaliyotangulia yaliyofanyika mwanzo wa mwaka (Januari/Februari), yatafanyika Juni 15 hadi Julai 13 mwaka 2019. Yatajumuisha mataifa 24.