Dondoo

Afichulia pasta jembe la mumewe halimfikishi Canaan

February 27th, 2019 1 min read

Na DENNIS SINYO

MOI’S BRIDGE, TRANS NZOIA 

Kalameni wa eneo hili, alimkemea mkewe vikali akidai alikuwa akimtangaza kanisani kwamba jembe lake lilikuwa limeshindwa kufanya kazi.

Jamaa alidai mkewe alimuanika kwa pasta wake ili apate ushauri. Kulingana na mdokezi, mwanamke huyo alimweleza pasta kwamba alikuwa ameshindwa kuvumilia maisha ya ndoa kwa sababu mumewe hangeweza kunguruma wakati wa tendo la ndoa.

“Mama alimwambia pasta kwamba mumewe hakuwa na umuhimu wowote isipokuwa kuchapa usingizi usiku wote,” alisema mdokezi.

Inadaiwa kwamba alilia machozi akiwa kwa pasta akisema alikuwa amechoka na ndoa.

Siku tatu baadaye, pasta huyo alimuita mume wa mama huyo ofisini mwake ili kujadili swala hilo. Bila kutarajia, jamaa alipigwa na mshangao alipopashwa kilio cha mkewe.

“Nimepata habari kwamba hulimi shamba jinsi inavyokupasa kama mume. Humfikishi mkeo Canaan,’’ alianza mhubiri huyo. Kabla ya kuendelea jamaa alisimama na kumfokea pasta akitaka kujua nani alimpasha hayo.

“Nani alikuelezea mimi nimeshindwa na kazi. Huyo mtu ni nani? Nataka kumjua!’’ aliteta kwa ukali.? Ilibidi pasta huyo kusema ukweli kwamba alikuwa amepokea ujumbe huo kutoka kwa mke wa jamaa.

“Ukweli nikwamba ripoti hizi zimetoka kwa mkeo. Analia kwamba shida hii imemkosesha amani kwa sababu hufanyi kazi yako,’’ alisimulia mhubiri huyo.

Jamaa huyo alisimama kwa mara nyingine na kuchomoka ofisini kwa fujo. ?Alipofika nyumbani, alimshtumu mkewe kwa? kumtangaza.

“Unajifanya kuwa mpole kumbe unaeneza maneno kwa watu wa kanisa. Kwa sasa kila mtu anajua kwamba mimi ninajikwaa, hio ni aibu gani jamani?’’ alifoka jamaa.

Yasemekana mkewe aliamua kutapika nyongo. “Mwanzoni ulikuwa mtu wa maana sana. Siku hizi huwezi chochote. Nimechoka na haya maisha,’’ alisema mkewe.

Mama huyo alimuonya mumewe na kutishia kumpa talaka akikosa kulima shamba kama zamani.