Makala

Afisa ashtuka aliyetaka kuoa kama mke wa pili ni kibiritingoma

May 29th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

AFISA mmoja wa ngazi ya juu katika idara ya polisi ameduwaa baada ya kupata ukweli wa mambo kwamba kidosho aliyekuwa amuoe kama mke wa pili ni kibiritingoma wa kawaida mtaani.

Afisa huyo anayehudumu mjini Mwea, Kaunti ya Embu, aligundua hayo baada ya yeye kukosana na mchumba wake huyo na katika hali ya kuridhiana, ilibidi wakubwa wa usalama eneo hilo waingilie kati.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ambazo wawili hao wameandikisha kama taarifa za kujieleza mbona wanalumbana, afisa huyo alifichua kwamba alikuwa amekutana na mwanamke huyo katika steji ya Sagana miezi mitatu iliyopita.

“Nilikuwa kwa gari langu siku moja na kufika katika steji hiyo jioni, nikamwona mwanamke huyo aliyevutia hisia zangu,” akasema afisa katika taarifa yake.

Aliongeza kwamba alisimamisha gari lake na baada ya kumhoji alikuwa akielekea wapi, ikaibuka kwamba wote wawili walikuwa na lengo la kufika katika mtaa jirani wa Makutano.

“Nilijitolea kumpa lifti na tukaanzisha gumzo hatua kwa hatua kiasi kwamba tuliafikiana tuingie kwa hoteli fulani na tukaagiza mvinyo,” akasema.

Afisa huyo alielezea kwamba mwanamke huyo alimwambia alikuwa akisaka kazi huku akiishi na dada yake katika viunga vya mji huo wa Makutano.
Siku ya kwanza kukutana na baada ya sherehe ya mvinyo, ripoti ilifichua kwamba mwanamke huyo hakusafiri hadi kwa dadake huyo, bali waliishia wote wawili hadi kwa nyumba ya afisa huyo.

Yaligeuka mazoea ya wawili hao kukutana na kupiga sherehe huku kilele kikiwa ni wawili hao kuingia kwa hiyo nyumba ya afisa.

Afisa huyo alisema kwamba aliweka ukweli wazi kwamba alikuwa na mke aliyekuwa akifanya kazi katika mji mwingine wa mbali.

“Lakini nilikuwa na nia ya kumuoa mwanamke huyo wa Makutano kwa kuwa penzi la dhati lilijengeka kati yetu, hata nikajitolea kumpa mtaji wa kuanzisha biashara,” akasema.

Mambo ya videge hao wawili ilienda sawa hadi mke wa afisa huyo alipotua katika mji wa Makutano na ikawa sasa huyo mpango wa kando kwanza akome kufika katika nyumba husika.

“Isitoshe, kulizuka changamoto ya kiusalama iliyohitaji polisi na maafisa kupekua madanguro na nilishtuka nilipomfumania mwanamke huyo akiwa uchi wa mnyama huku akirushana roho na mteja. Ndani ya danguro kulikuwa kumejaa kondomu zilizokuwa zimetumika,” akasema.

Alieleza kuwa ule mshtuko aliopata uligeuka ghafla kuwa hasira iliyoishia yeye kumzaba mwanamke huyo kofi na akatoka kwa chumba hicho hata bila kumkamata.

Kwa upande wake mwanamke huyo, alienda kwa wakubwa wa afisa huyo kuripoti kwamba alichapwa na akatishiwa uhai, akidai alipwe fidia ya Sh50,000.

Ni katika hali hiyo ambapo afisa huyo alijitetea akisema licha ya kujuta kupandwa na hasira, kisa hicho kikadiriwe kama cha wapenzi walioingia katika mzozo wa kawaida.

Alisema kwamba angekuwa na nia mbaya na maisha ya mwanamke huyo, angemkamata na ahakikishe amefungwa gerezani.

“Aidha, katika kazi yangu, ni wazi kwamba ningekuwa na mbinu kadha za kumsababishia madhara lakini sikuwazia ukatili huo na hadi sasa nimetulia, nimepoa na nimekubali hali ilivyo kwamba niliyempenda ni kahaba tu wa kawaida mtaani,” akasema afisa huyo.

Kesi bado haijaamuliwa.

[email protected]