Habari Mseto

Afisa kurudishia wakazi 2,200 wa Mukuru shamba la Sh1b

May 13th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KINARA wa shirika la kustawisha makazi ya wakazi wa mitaa ya mabanda Bi Jane Weru Jumatatu alieleza mahakama kuu yuko tayari kuwapa wakazi 2,221 wa Mukuru hati miliki ya shamba walililonunua miaka 12 iliyopita, na lenye thamani ya Sh1 bilioni.

Bi Weru, ambaye ni afisa mkuu wa muungano wa wanavijiji, Akiba Mashinani Trust (AMT), alimsihi Jaji Elijah Ombaga azingatie maslahi ya wanachama wote wa Mukuru Makao Bora Trust akitoa uamuzi wake.

“Naomba hii mahakama izingatie maslahi ya wanachama wote wa Mukuru Makao Bora Trust inapotoa uamuzi wa kesi hii,” alisema Bi Weru.

Wakazi hao walinunua shamba hilo kupitia kwa AMT lakini Bi Weru amekataa kuwapa hati miliki ndipo wastawishe nyumba zaidi ya 3,000 za wakazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru ulioko kaunti ndogo ya Embakasi, Nairobi.

Bi Weru aliyehojiwa na wakili Timothy Grant alitoa historia jinsi wanakijiji hao walipochanga zaidi ya Sh72 milioni na AMT ikawasaidia kupewa mkopo na Benki ya Eco Bank.

Mahakama ilielezwa Benki hiyo iliwapa mkopo wa Sh55 milioni kumlipa mwekezaji aliyeuza shamba hilo kwa bei ya Sh81milioni.

“Wakazi hawa wa Mukuru walimaliza kulipa mkopo huo katika muda wa miezi 19,” alisema Bi Weru.

Bi Weru alisita alipokuwa anohojiwa na wakili Ramadhan Abubakar kuhusu Sh23milioni anazodai kutoka kwa wanachama hao.

Mhasibu wa AMT Bw Leonard Waringa hakuwasilisha taarifa ya akaunti ya Mukuru katika benki hiyo ya Ecobank.

Bw Waringa aliyeajiriwa na kampuni ya Uhasibu ya Labonyo & Associates alihojiwa na wakili Ramadhan Abubakar na hakuwasilisha ripoti ya akaunti ya wakazi hao wa kijiji cha Mukuru.

Wanachama wa Mukuru Makao Bora walilalamika kesi kuahirishwa kwa muda mrefu lakini Bw Abubakar akawashauri wawe na subira.

Kesi itaendelea Oktoba 17.