Afisa mwingine wa ODM apata Covid-19

Afisa mwingine wa ODM apata Covid-19

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kulazwa hospitalini kwa kuugua Covid-19, mkurugenzi wa chama hicho Philip Etale naye amepatikana na virusi vya ugonjwa huo.

Akitangaza kuhusu hali yake ya kiafya, Bw Etale hata hivyo alielezea matumaini kuwa atapona na kurejelea maisha yake ya kawaida.

“Nimepatikana na virusi vya corona. Japo nimeponzwa, ningali na matumaini kuwa nitashinda. Nitapona. Mniombee, marafiki. Kwa Mungu Naamini,” akaandika katika akaunti yake ya Twitter.

Jumatano, Bw Odinga alipatikana na corona baada ya kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Nairobi.

Hata hivyo, daktari wake, David Olunya, alisema mwanasiasa huyo mkongwe yuko katika hali nzuri huku akipokea matibabu. Bw Odinga alisema atasalia karantini hadi wakati madaktari wake wataamua arejee nyumbani.

Waziri huyu mkuu wa zamani na Bw Etale wanafikisha idadi ya viongozi wa ngazi ya juu katika ODM ambao wameambukizwa Covid-19 tangu ilipolipuka 2020 kuwa watatu.

Wa kwanza alikuwa ni Kiongozi wa Vijana katika ODM Benson Musungu.

You can share this post!

Tangatanga washabikia ‘uhasla’ wa Rais Biden

TAHARIRI: Miungano yote ya kisiasa izingatie sera