Michezo

Afisa wa Galatasaray kuzungumza na Spurs kuhusu Wanyama

August 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SIKU nne baada ya kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza kufungwa Agosti 9, ripoti kutoka nchini Uturuki zinasema kuwa mmoja kati ya viungo wakabaji Mkenya Victor Wanyama (Tottenham Hotspur) na Mfaransa Tiemoue Bakayoko (Chelsea) wako kwenye rada ya Galatasaray.

Tovuti ya Sport Witness inasema kuwa afisa kutoka Galatasaray, Sukru Haznedar yuko jijini London kwa mazungumzo.

Mauricio Pochettino alipendezwa na soka ya Wanyama na kumleta Southampton mnamo Julai mwaka 2013 na kisha Tottenham Juni mwaka 2016.

Hata hivyo, baada ya kukosa huduma za nahodha huyo wa Harambee Stars katika mechi nyingi kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya magoti katika msimu hiyo miwili iliyopita, kocha huyo kutoka Argentina alionyesha kumshiba Wanyama aliposaini viungo Tanguy Ndombele na Giovani Lo Celso.

Ripoti katika tovuti Sport Witness nchini Uturuki zinasema sasa kuwa mmoja kati ya Wanyama na Bakayoko atajiunga na miamba wa Galatasaray.

Big Vic, jinsi Wanyama anafahamika kwa jina la utani, alihusishwa na uhamisho hadi Galatasaray na Fenerbahce nchini Uturuki na West Ham, Burnley, Brighton, Wolves na Southampton nchini Uingereza katika kipindi kirefu cha uhamisho.

Hakuna klabu yoyote nchini Uingereza ilimtafuta katika kipindi hicho kilichofunguliwa nchini Uingereza mnamo Mei 17 na kutamatika Agosti 9.

Hii iliwacha uwanjani klabu nje ya Uingereza kutafuta huduma zake, huku zile za kuelekea Fenerbahce zikififia kabisa. Amehusishwa pia na klabu ya Celtic aliyoichezea na kupata umaarufu wa kutosha kumfanya avutie Pochettino aliyemfanya kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alipojiunga na Southampton.

Mara ya kwanza ripoti ziliibuka kuwa Spurs inataka kuuza Wanyama ilikuwa Januari mwaka 2019, lakini kipindi hicho kifupi cha uhamisho kilikamilika akiwa bado katika klabu hiyo kutoka jijini London.

Uvumi kuwa Wanyama anaondoka Tottenham katika kipindi kirefu cha uhamisho uliongezeka hata zaidi baada ya klabu yake kukamilisha msimu wake ilipokutana na Liverpool katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mnamo Juni 1 nchini Uhispania, ingawa tena kilipita nchini Uingereza akiwa bado hajapata klabu nyingine.

Kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uturuki na Scotland kitafungwa Septemba 1. Ikipita Septemba 1, basi uwezekano wa Wanyama kusalia mchezaji wa Tottenham msimu 2019-2020 utakuwa mkubwa kwa sababu hakuna ripoti kuwa amevutia klabu nchini Urusi, Romania, Bulgaria, Uholanzi, Ufaransa, Uhispania na Italia ambazo zitafunga milango yao kati ya Septemba 2 na Septemba 8.