Afisa wa GSU aangamiza wenzake wawili kwa risasi na hatimaye kujiua Trans-Nzoia

Afisa wa GSU aangamiza wenzake wawili kwa risasi na hatimaye kujiua Trans-Nzoia

Na SAMMY WAWERU

HALI ya huzuni imetanda katika kambi ya maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) ya Chepchoina, Kaunti ya Trans-Nzoia baada ya afisa mmoja kuua wenzake wawili kwa kuwapiga risasi Jumanne jioni kisha akajitia kitanzi.

Kulingana na taarifa ya idara ya polisi, afisa huyo aliyetambulika kama Bw Paul Kuria alifyatua risasi kiholela, tukio ambalo lilisababisha maafa ya maafisa wawili na kadha kujeruhiwa.

“Baadaye alijipiga risasi kupitia chini ya kidevu, akafa papo hapo,” inaeleza taarifa ya polisi.

Aidha, inasemekana hakukuwa na ugomvi wowote kati ya afisa huyo na wenzake, kabla kutekeleza tukio.

“Uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha kitendo hicho,” idara ya polisi imesema.

Visa vya maafisa wa usalama kuua wenzao na pia raia vinaendelea kushuhudiwa.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, 2020 na mwanzoni mwa mwaka huu, visa kadha vya maafisa wa polisi kuangamiza wenzao na pia raia viliripotiwa katika Kaunti ya Nairobi na Kirinyaga.

You can share this post!

FC Porto yaangusha miamba Juventus kwenye soka ya UEFA...

NDIVYO SIVYO: Matumizi uchwara ya kiunganishi ‘kama...