Afisa wa KDF akiri kupokea hongo ya Sh2.4 milioni kusaidia watu sita kujiunga na idara ya polisi

Afisa wa KDF akiri kupokea hongo ya Sh2.4 milioni kusaidia watu sita kujiunga na idara ya polisi

NA RICHARD MUNGUTI

AFISA wa Jeshi (KDF) Antony Barongo Buge amekiri katika Mahakama ya Milimani Nairobi kwamba alipokea hongo ya Sh2.4 milioni kusaidia watu sita kupata kazi katika kikosi cha polisi.

Akihojiwa na wakili Danstan Omari katika kesi ambapo Nelson Mukara Sichere ameshtakiwa kughushi barua ya Naibei Sharon Chemtai kujiunga na Taasisi ya Mafunzo ya Polisi (NPTC), Barongo mwenye umri wa miaka 42 alikiri “nilipokea Sh2.4 milioni Aprili 2022 kufanikisha watu sita kujiunga na idara ya magereza.”

“Kutokana na ushahidi wako wewe ni mmoja wa genge la majambazi katika KDF wanaowalaghai wananchi pesa wanapotafuta kazi ya kujiunga na vikosi vya usalama,” Bw Omari alimwuliza Barongo aliyetoa ushahidi mbele ya hakimu mkazi Gilbert Shikwe, Mahakama ya Milimani Nairobi.

“Nilipokea pesa hizo kisha nikampa Sichere kufanikisha walalamishi kujiunga na idara ya magereza,” Barongo anayehudumu katika chuo cha Lanet alijibu.

Aliongeza kusema alikabidhiwa barua ya Chemtai na Bw Sichere katika hoteli ya Pumbkin iliyoko Kilimani, Nairobi akiandamana na Bi Ashley Ayuma mnamo Aprili 27, 2022.

Bw Sichere amekana mashtaka mawili ya kughushi barua ya kujiunga na idara ya polisi akidai imetayarishwa na NPS ya kumteua Chemtai kujiunga na chuo cha kutoa mafunzo kwa polisi-Kiganjo.

Barongo alieleza hakimu alimkabidhi Bw Sichere pesa hizo katika hoteli za Pumbkin na Ole Sereni.

“Ashley alienda Kiganjo na ikathibitishwa barua iliyotoka kwa Sichere kubaini kama ilikuwa feki,” Bw Omari alimwuliza Barongo.

“Ndio Ashley Ayuma alienda Kiganjo na ikathibitishwa barua aliyokabidhiwa na Sichere ilikuwa feki,” Barongo alijibu.

Bw Shikwe alielezwa na Bw Omari, kitendo cha Barongo kimefedhehesha maafisa wa KDF wanaosifika kudumisha amani maeneo mbali mbali ulimwenguni.

Licha ya kupokea pesa hizo, Barongo alisema hajawahi kufunguliwa mashtaka.

Kesi itaendelea Februari 28, 2023.

Sichere amekanusha mashtaka mawili ya kughushi barua za kujiunga na idara ya polisi.

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza sasa kuvaana na Senegal...

Msasa wa mawaziri wa Sakaja kuendelea

T L