NA RICHARD MUNGUTI
AFISA wa polisi aliyekosa kufika kortini kujibu mashtaka ya mauaji ya vijana wawili mtaani Eastleigh jijini Nairobi, ameagizwa ajisalamishe katika kituo cha polisi cha Garissa mara moja.
Endapo hatajisalimisha kwa DCIO Garissa, Sajini Ahmed Rashid aliamriwa ajisalamishe kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Japeth Koome Januari 26, 2023.
Jaji Kanyi Kimondo aliyetoa maagizo hayo pia alimwamuru wakili Danstan Omari awasilishe mara moja kesi ya kupinga Sajini Rashid akifunguliwa mashtaka ya kuwaua Jamal Mohamed na Dahir Kheri mnamo Machi 31, 2017 mtaani Eastleigh, Nairobi.
Jaji Kimondo alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Saj Rashid hakufika kortini kama alivyoagizwa Desemba 2022 afike kortini Januari 26, 2023 kujibu mashtaka ya mauaji kwa vile alikuwa amesafiri hadi Garissa kushughulikia dharura ya familia.
Sajini Rashid atashtakiwa kwa mauaji ya Jamal Mohamed na Dahir Kheri mnamo Februari 9, 2023.
Wakili Danstan Omari aliagizwa awakabidhi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na nakala za ombi hilo la kupinga kesi hiyo kabla ya Feburuari 8, 2023 kesi itakapotajwa kwa maagizo zaidi.