Habari

Afisa wa polisi akana kumuua mwanafunzi wa darasa la nane

June 23rd, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi ameshtakiwa Jumanne kumuua mwanafunzi wa darasa la nane Yassin Hussein Moyo miezi mitatu iliyopita alipokuwa akitekeleza sheria za kafyu.

Jaji Luka Kimaru ameamuru Duncan Ndiema Ndiwah almaarufu Champs azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Capitol Hill hadi kesho Jumatano ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana litakaposikizwa.

Ndiwah alikana alimuua Yassin alipokuwa akishika doria pamoja na maafisa wengine wa polisi kuhakikisha wananchi wametii amri ya kutotoka nje baada ya saa moja jioni iliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta ili kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Yassin alikuwa amesimama kwenye dari la nyumba yao iliyoko Kiamaiko mtaani Huruma, Kaunti ya Nairobi. Alikuwa katika orofa ya tatu akisimama pamoja na dada zake na mama yake alipopigwa risasi.

Ndiwah aliyetarajiwa kufika kortini Ijumaa wiki iliyopita hakufika kwa vile ilidaiwa alienda katika hospitali mojawapo kupimwa ikiwa ana ugonjwa wa Covid-19.

“Mshtakiwa hakufika kortini Ijumaa kama alivyokuwa ameamriwa wiki mbili zilizopita na Jaji Jessie Lesiit kwa sababu alikuwa ameenda kupimwa ikiwa yuko na virusi vya corona,” Jaji Kimaru amefahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Gikui Gichuhi.

Ripoti kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan alikokaguliwa imeonyesha mshtakiwa hana Covid-19.

“Mshtakiwa hana corona kulingana na ripoti ya hospitali ya Aga Khan,” Bw Omari amedokeza.

Jaji Kimaru amehoji ikiwa kiongozi wa mashtaka Bi Gichuhi alikuwa anapinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bi Gichuhi amesema atapinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana lakini akaomba apewe muda awasilishe hati ya kiapo inayosimulia sababu za kupinga dhamana hiyo.

Wakili Danstan Omari, Anita Masaki na mawakili wengine sita wanaomtetea mshtakiwa wamemweleza Jaji Kimaru kwamba tayari wamewasilisha katika sajili ya Mahakama Kuu ombi la kuachiliwa kwa dhamana kwa mshtakiwa.

“Nitamkabidhi Bi Gichuhi nakala ya ombi la mshtakiwa la kutaka aachiliwe kwa dhamana,” amesema Bw Omari.

Jaji Kimaru atasikiza ombi hilo kesho Jumatano.