Habari Mseto

Afisa wa Safaricom aomba msamaha kwa kukosa kumfikisha kortini mtaalamu

February 14th, 2018 1 min read

Wafanyazikazi wa Safaricom Mhandisi Henry Siongok (kushoto) , Inspekta Henry Rabala (kati) na mwakilishi wa mkurugenzi mkuu (kulia) wakiwa mahakamani Jumanne. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa masuala ya kisheria wa kampuni ya Safaricom Jumanne aliomba mahakama msamaha kwa kukosa kumwasilisha kortini mtaalamu wa masuala ya mawasiliano kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili raia mmoja wa Tanzania, Charles Rashid anayeshtakiwa pamoja na wengine wanne kwa mauaji ya wanafunzi 147 wa Chuo Kikuu cha Garissa Aprili 2, 2015.

Wakili wa Safaricom, Bi Kweya alikana madai Safaricom iko na njama za kuhujumu kesi dhidi ya washukiwa hao watano wa ugaidi.

Hakimu mkuu Francis Andayi alisema maafisa hao watano ni jambo mbaya. “Hii mahakama iliambiwa kati ya Desemba 2017 na Feburuary 13 2018 mmekataa katakata kujibu mawasiliano yote kutoka kwa kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu,” Bw Andayi aliwaambia wafanyakazi hao.

Baada ya kuomba msamaha Bi Kweya alisema Mhandisi Siongok atafika kortini Alhamisi kutoa ushahidi katika kesi hiyo dhidi ya Bw Rashid, Mohamed Abdikar, Hassan Aden Hassan, Sahal Diriyena na Osman Abdi.

Wafanyakazi hao waliogopa mno walipokuwa kizimbani kwa vile hawakujua hatua watakayochukuliwa.