Habari Mseto

Afisa wa ujasusi ajitoa uhai kwa risasi ya kichwani

June 5th, 2024 1 min read

NA STEVE OTIENO

AFISA mkuu wa Idara ya Ujasusi (NIS) alijitoa uhai kwa kujipiga risasi kichwani akiwa nyumbani kwake Kilimani, Nairobi.

Rekodi za polisi zilionyesha kuwa mpwa wa Bw Tom Mboya Adala aliyekuwa Naibu mkurugenzi wa NIS katika makao makuu ya Ruaraka, alijipiga risasi upande wa kulia wa kichwa na ikatokea upande wa kushoto.

Rekodi hizo zilionyesha kuwa mpwa wa marehemu, Francis Oduor, aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Kilimani kuwa alimwona mjomba wake mara ya mwisho Juni 3, 2024 mwendo wa saa nne usiku alipokuwa akienda kulala.

Hata hivyo alijua mambo si sawa siku iliyofuata saa tatu asubuhi baada ya kumkosa marehemu.

“Aliyepiga ripoti, alienda katika chumba chake lakini hakuwepo. Alimuuliza mlinzi iwapo marehemu alikuwa ametoka nje lakini hajatoka,” ilisema ripoti hiyo.

Bw Odour, alianza kuzunguka kweye boma hilo, kuchunguza alipo mjombaye na kisha kumpata akiwa amelala ndani ya nyumba za wafanyakazi.