Habari

Afisi ya DCI ina mamlaka ya kuchunguza kesi za ufisadi – Kihara

April 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MWANASHERIA Mkuu Paul Kihara amemtetea Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti dhidi ya madai kuwa hana mamlaka ya kikatiba kuendesha uchunguzi kuhusu kesi za ufisadi.

Akihutubu Jumanne alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) Bw Kihara alisema alisema DCI ana mamlaka ya kuchunguza kesi za ufisadi ambazo alisema zinazoorodheshwa kama uhalifu wa kiuchumi.

“Katiba na Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi zinampa DCI wajibu wa kuchunguza kesi zote za ufisadi,” Bw Kariuki akasema.

“Kimsingi, ufisadi ni uhalifu na hauwezi kuelezewa kwa njia nyingine. DCI na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) wana wajibu wa kuchunguza kesi za ufisadi,” akaongeza.

Sehemu ya 4 (35) ya Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inasema kuwa DCI atakusanya habari za kijasusi, atafanya uchunguzi kuhusu kesi mbalimbali za uhalifu kama kama vile mauaji, ulanguzi wa dawa za kulevya, ulanguzi wa watu, ulanguzi wa fedha, ugaidi,”

Bw Kihara alikuwa ameandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak ambaye pia alitetea DCI kuhusiana na wajibu wake wa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) ana mamlaka ya kuchunguza aina yoyote ile ya uhalifu, na haijalishi aina ya uhalifu,” Bw Mbarak akaambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo.

Kauli ya Bw Kihara ambaye ni mshauri mkuu serikali katika masuala ya kisheria inakinzani na ile ambayo ilitolewa mwezi jana na Naibu Rais William Ruto akisema kuwa Bw Kinoti hana mamlaka ya kikatiba kuchunguza kesi za ufisadi.

Akiongea katika kijiji cha Kapng’etuny katika eneo bunge la Ainamoi, Dkt Ruto alisema sheria haimruhusu DCI kuchunguza kesi za uhalifu wa kiuchumi, akiongeza kuwa kesi hizo zinapasa kushughulikiwa na EACC.

“Vita dhidi ya ufisadi lazima ziendeshwe kwa misingi ya uelewa wa kisheria na asasi yenye uwezo na mamlaka ya kikatiba. Na asasi hiyo ni EACC wala sio DCI wala DPP,” Dkt Ruto akasema

Naibu Rais alikuwa amehudhuria hafla ya kusherehekea ushindi wa Mbunge wa eneo hilo Silvanus Maritim, shughuli ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Kawi Charles Keter na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao.