Habari Mseto

Afisi ya Kadhi yakerwa na ongezeko la talaka

September 5th, 2019 2 min read

MISHI GONGO na KALUME KAZUNGU

KADHI Mkuu Sheikh Muhdhar Ahmed amewahimiza wazazi kote nchini wawape mafunzo vijana kuhusu maisha ya ndoa, ili kuepuka talaka zinazoshuhudiwa kwa wingi nchini.

Aidha, alisema kuwa hata ingawa wazazi wana kauli katika masuala ya ndoa za watoto wao, wanapaswa kutekeleza jukumu la ushauri pekee na wala si kuwalazimisha vijana kuoa au kuolewa na watu ambao hawajawachagua.

Alisema kesi nyingi zinazowasilishwa katika mahakama ya Kadhi ni zile za wanaume wanaofanya kazi katika mataifa ya kigeni, mbali na wake wao.

Alisema mahusiano kati ya wanandoa wanaoishi masafa marefu na wapenzi wao huchangia mwanamke au mwanamume kushiriki katika zinaa, jambo linalochangia kusambaratika kwa ndoa.

Aliwalaumu wazazi wanaowalazimisha mabinti zao kuingia katika ndoa ili kuepuka aibu za mabinti hao kujihusisha katika mahusiano yanayoleta mimba za nje ya ndoa.

“Kuna wazazi pindi wanapoona mtoto wa kike amebalehe humtafutia mchumba na kumuoza pasi kumshauri; matokeo yake ni talaka za ndoa changa,” alisema.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka wa 2017 ndoa zilizosajiliwa zilikuwa 909 nazo talaka zikawa 244, Mwaka 2018 ndoa zilikuwa 1033 na talaka 233.

Kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, afisi ya Kadhi imesajili, talaka 160. Kadhi Mkaazi Mwandamizi Habib Salim, aliwalaumu wazazi kwa kukosa kuwapa mafunzo vijana wao kabla ya kuingia katika ndoa hivyo kuwaacha kupata mafunzo kutoka kwa sinema, kwenye televisheni na marafiki.

Alieleza kuwa awali vijana walilazimika kupitia mafunzo ya jinsi ya kuishi katika ndoa, lakini kizazi cha sasa kimetupilia mbali tamaduni hiyo.

“Mabinti huangalia sinema za Kihindi na zile za Kimexico bila kuzingatia kuwa wanachofanya ni biashara, mabinti huiga na kuamini kuwa hayo ndiyo mapenzi, hivyo kusisitiza waume wao kuwapa mapenzi ya filamu,” alisema. Kadhi Salim alisisitiza kuwa vijana wengi hushindwa kuwatimizia wanawake wao mahitaji ya kimwili hali inayochangia talaka.

“Vijana wengi wana mazoea ya kupoteza wakati wao maskani; ukosefu wa mafunzo huwafanya vijana hawa kutobadili mienendo yao hata baada ya kuoa, hili na matumizi ya vileo vinavyowakosesha hamu za wake wao hivyo kuwanyima tendo la ndoa,” alisema.

Alieleza mbeleni kuwa wanawake walikuwa wanyenyekevu na wanaume walikuwa na busara lakini kupitia kampeni zinazoendelezwa duniani za kutafuta haki za wanawake, wake wamesahau kunyenyekea, hivyo kusababisha vita na majibizano kati ya wanandoa.

Katika Kaunti ya Lamu, zaidi ya nusu ya ndoa zinazofungishwa huvunjika. Kadhi Mkazi wa Mahakama ya Lamu, Bw Swaleh Mohamed, anasema ni asilimia 40 pekee ya ndoa za Lamu ambazo zimesajiliwa ilhali asilimia 60 ya ndoa hizo zikiwa hazitambuliwi kisheria.

“Nawasihi wanandoa wathamini ndoa zao na kuepuka talaka. Pia waje ofisini kusajili ndoa zao badala ya kuendelea kuishi gizani,” akasema Bw Mohamed.