HabariSiasa

Afisi yangu ipewe mamlaka zaidi – Ruto

February 9th, 2019 3 min read

CAROLYNE AGOSA na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto sasa anataka afisi yake ipewe mamlaka zaidi huku Rais akidumisha mamlaka makuu, na kuzidi kupinga kuundwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza Ijumaa nchini Uingereza, Dkt Ruto alipendekeza muundo wa serikali ya kitaifa ufanyiwe mabadiliko ili kuwa na Afisi ya Rais na Afisi ya Upinzani.

Katika mapendekezo yake, Dkt Ruto anataka Afisi ya Rais isalie kuwa na mamlaka makuu kama ilivyo sasa ambapo rais ndiye kiongozi wa serikali.

Aidha, Dkt Ruto anataka kuundwa kwa Afisi ya Kiongozi wa Upinzani itakayoongozwa na kinara wa chama ama muungano wa vyama ambao mgombea wake wa urais ataibuka wa pili kwenye uchaguzi mkuu.

“Baada ya kinara wa upinzani kutwaa wadhifa wa upinzani rasmi bungeni, naibu rais anafaa kutwaa uongozi wa shughuli za serikali bungeni,” Dkt Ruto aliambia wajumbe kwenye mhadhara ulioandaliwa katika jumba la Chatham House mjini London.

Msimamo huu mpya wa Dkt Ruto unajiri siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumpa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i mamlaka zaidi ya kusimamia miradi ya serikali, hatua ambayo ilionekana kupunguza mamlaka ya Naibu Rais.

Dkt Ruto sasa anataka afisi yake ipewe nguvu za kusimamia shughuli zote za serikali bungeni, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni Adan Duale.

Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamekuwa wakipendekeza kupanuliwa kwa serikali ili kuhakikisha jamii zote zimewakilishwa, kauli ambayo Dkt Ruto anaonekana kupinga.

Akiunga mkono mjadala unaoendelea nchini kuhusu marekebisho ya katiba yatakayojumuisha rasmi viongozi wa sasa wa upinzani serikalini, Naibu Rais alisema mfumo wa sasa umeshindwa kukuza ipasavyo uwajibikaji serikalini na badala yake umeipa demokrasia yetu upinzani butu.

Alisisitiza kuwa suluhisho sio= kinara wa upinzani kupewa wadhifa wa Waziri Mkuu unaoandamana na manaibu wawili.

Badala yake, Dkt Ruto anataka kinara huyo wa upinzani pamoja na mgombea wake mwenza wote wafanywe wabunge moja kwa moja, na kutwaa uongozi wa Upinzani Rasmi.

“Siungi mkono wanaopendekeza kuundwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka kwa sababu hatua hiyo haitasuluhisha changamoto tunazokabiliana nazo,” akasema.

“Si sawa kwa kinara wa chama kinachoibuka cha pili kwenye uchaguzi mkuu kukosa wadhifa rasmi kikatiba. Chaguzi nchini Kenya huwa na ushindani mkali. Mara nyingi, mshindi na mpinzani anayechukua nafasi ya pili huwa wamejizolea kura zaidi ya milioni tano. Halafu mshindi anatwaa wadhifa uliopewa mamlaka rasmi huku nambari mbili akiachwa hohehahe,” alieleza Dkt Ruto.

Hata hivyo, ametilia shaka iwapo taifa hili liko tayari kwa kura ya maamuzi akiashiria kuwa hakuna fedha za kuandaa shughuli hiyo.

Dkt Ruto alikiri kuwepo kwa masuala yanayohitaji marekebisho ya katiba, hata hivyo, alitilia shaka iwapo muda wa kufanya marekebisho hayo umewadia hususan ikizingatiwa kuwa taifa hili linajiandaa kwa shughuli tatu kuu za kitaifa katika miaka mitatu ijayo.

“Ndiyo, kuna mambo (ya kurekebishwa) katika katiba. Lakini je, tumefikia upeo wa hitaji letu la kutaka kura ya maamuzi? Je, tufanye kura ya maamuzi pamoja na uchaguzi mkuu?” akauliza Dkt Ruto.

Aliongeza: “Je, kuna fedha za kuandaa Sensa ya kitaifa mwaka huu, kisha ukaguzi mpya wa mipaka ya maeneo-bunge mwaka ujao (2020), halafu ifuate kura ya maamuzi pamoja na uchaguzi mkuu?”

Dkt Ruto alisisitiza hilo si suluhu na kusema kuwa “siamini kwamba tuna wawakilishi kupita kiasi.”

Wakati huo huo, Dkt Ruto alisema hatamjibu aliyekuwa Naibu Mwenyeketi wa Jubilee David Murathe ambaye amekuwa akimpiga vita vya kisiasa tangu Desemba mwaka jana.

Akijibu maswali kutoka kwa wanahabari baada ya kuhutubu katika mhadhara wa kila mwaka katika ukumbi wa Chatham House, Dkt Ruto alisema Murathe si mtu wa hadhi yake.

“Sijamjibu Murathe nchini Kenya, sitamjibu hapa Uropa, hastahili jibu langu,” akasema.

Bw Murathe alianza kumshambulia Dkt Ruto mwishoni mwa mwaka jana alipodai kuwa naibu huyo wa rais anapaswa kustaafu pomoja na Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2022.