Kimataifa

Afisi za upinzani zapakwa kinyesi uchaguzi ukinukia

August 1st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

ZAIDI ya afisi 10 za chama kikuu cha upinzani nchini Burundi zimepakwa kinyesi cha binadamu na zingine kuteketezwa ndani ya muda wa mieizi miwili iliyopita, afisa mmoja wa chama jana aliwaambia wanahabari.

Therence Manirambona, ambaye ni msemaji wa chama cha National Congress for Freedom (CNL), alisema kitendo hicho ni sehemu ya juhudi za kuhujumu demokrasia na kuutisha upinzani kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka ujao, 2020.

Wizara ya Masuala ya Ndani haijasema lolote kuhusiana na visa hivyo.

Msemaji huyo wa CNL alisema, afisi ya hivi punde kushambuliwa kwa kinyesi na kisha kuteketezwa ni ile iliyoko katika mji wa Gatete, magharibi mwa wilayani Rumonge.

Bw Manirambona alisema kufikia sasa waliotekeleza kitendo hicho hawajulikani kwa sababu maafisa wa serikali hajaanzisha uchunguzi wowote.

“Kitendo cha kupaka afisi zetu kwa kinyesi cha binadamu ni dhuluma kubwa kupitia kiasi,” akasema.

“Tunashuku kuwa vitendo kama hivi vimechochewa kisiasa. Hii ni kwa sababu katika maeneo ya mashinani viongozi wengine wa kisiasa wanaamini chama chetu cha CNL hakipaswi kuwa na afisi katika maeneo yao,” Bw Maniramba akaongeza.

Mwezi jana, maafisa wa uchunguzi kutoka Tume ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Haki za Kibinadamu walitoa ripoti iliyoelezea kwa mapana kuhusu “vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu vinavyotendewa upinzani nchini Burundi.”

Kulingana na ripoti hiyo, angalau watu watatu waliuawa, wanne wakatoweka na jumla ya 24 wakamatwa kwa kukisiwa kuwa wanachama wa CNL katika mikoa minane nchini Burundi kuanzia Januari mwaka huu.

Vile vile, ripoti ya UN ilisema watu wengine watatu waliuawa na mmoja akatoweka katika maeneo wanakoishi wafuasi wengi wa upinzani.

Lakini siku chache baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo mwakilishi wa Burundi katika tume ya UN yenye makao yake jijini Geneva, Uswizi aliitaja ripoti hiyo kama “stakabadhi yenye uwongo”.

Mnamo 2015, Burundi ilitumbukia katika ghasia za kisiasa wakati Rais Pierre Nkurunziza alitangaza kuwa angewania urais kwa muhula wa tatu. Wafuasi wa upinzani walifanya maandamano kupinga hatua hiyo wakisema ilikwenda kinyume na sheria.

Miaka mitatu baada ya ghasia hizo kura ya maamuzi ilifanyika ambapo wananchi waliidhinisha mabadiliko ya katiba.