Afrika huagiza kiwango kikuu cha fatalaiza, matumizi yakiwa chini – Ripoti

Afrika huagiza kiwango kikuu cha fatalaiza, matumizi yakiwa chini – Ripoti

NA SAMMY WAWERU

AFRIKA hununua nje ya Bara kiwango kikubwa cha mbolea ila matumizi yake ni ya chini, yakilinganishwa na mabara mengine ulimwenguni.

Kulingana na ripoti ya utafiti wa hivi punde wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Mikakati ya Chakula (IFPRI), kiwango cha fatalaiza inayotumika Afrika ni chini ya asilimia nne ya idadi jumla inayoundwa ulimwenguni.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliotolewa kupitia warsha iliyoandaliwa na Muungano wa Sasakawa Afrika (SAA), virutubisho vyote; Nitrojini, Potasiamu na Kalsiamu vikijumuishwa matumizi ni kati ya tani milioni 190 – 200.

“Afrika inatumia tani milioni 7 pekee, thuluthi moja ya kiwango hicho ikitumika katika nchi za Afrika Kaskazini,” akasema Dkt David Laborde, mtafiti kutoka IFPRI wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Matokeo ya utafiti huo yanatahadharisha na kuzua hofu ya upungufu wa chakula duniani na hata mfumko wa bei, kufuatia mgogoro unaoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Vita kati ya nchi hizo mbili vimesababisha gharama ya mbolea kupanda, Dkt Laborde akisema wakulima wa mashamba madogo ndio wanaumia zaidi.

Urusi ndio mzalishaji mkuu wa fatalaiza katika ngazi ya kimataifa, na vikwazo ilivyowekewa na baadhi ya mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani vimechangia mfumko wa bei.

Isitoshe, bei ya gesi – kiungo muhimu katika utengenezaji wa mbolea imepanda mara dufu viwanda vikikiri kulemewa hivyo basi kuathiri uundaji na usambazaji.

Hata kabla ya kero ya kupanda kwa bei inayogubika Afrika, Dkt Laborde anasema Bara hili pia lilikuwa chini kimatumizi na kiuzalishaji.

Huku utafiti huo ukijiri, Naibu wa Rais Kenya, Bw Rigathi Gachagwa jana alizindua rasmi usambazaji wa mbolea ya bei nafuu.

Hatua hiyo inatokana na ahadi ya Dkt William Ruto baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya, kutoa ruzuku ili kusaidia kushusha bei ya mbolea nchini.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Wakati mwingine tuache ujinga

Gavana Mwadime alenga utalii kuinua uchumi wa Kaunti

T L