Michezo

Afrika Kusini ni wafalme wa Dubai Sevens 2019, Kenya yamaliza nambari 13

December 7th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFRIKA Kusini ndio mabingwa wa duru ya ufunguzi ya Raga za Dunia za wachezaji saba kila upande baada ya kuchabanga mabingwa watetezi New Zealand 15-0 mjini Dubai, Jumamosi.

Mabingwa mara tatu wa dunia Afrika Kusini, ambao walikuwa wameshinda Dubai Sevens mara ya mwisho mwaka 2017 walipobwaga New Zealand 24-12 katika fainali, walizamisha washikilizi hao wa mataji mengi ya dunia kupitia miguso ya Siviwe Soyizwapi, Chris Dry na Seabelo Senatla.

Afrika Kusini, ambayo itaandaa duru ya pili mjini Cape Town mnamo Desemba 13-15, inaongoza msimu kwa alama 22. Mabingwa mara 12 wa dunia New Zealand walikamilisha ziara ya Dubai Sevens kwa alama 19, mbili mbele ya Uingereza iliyonyuka Samoa 19-17 katika mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba.

Wafalme wa Singapore Sevens mwaka 2016 Kenya, ambao walilemewa na Afrika Kusini 17-12 na Uingereza 12-5 katika mechi za Kundi D mjini Dubai, walikamilisha kampeni yao kwa kulima Scotland 26-14. Vijana wa kocha Paul Feeney walikusanya alama nne kutoka duru hiyo ambayo walimaliza katika nafasi ya 13.

Msimamo wa Raga za Dunia za msimu 2019-2020 baada ya Dubai Sevens:

1. Afrika Kusini (alama 22),

2. New Zealand (19),

3. Uingereza (17),

4. Samoa (15),

5. Australia (13),

6. Ufaransa (12),

7. Argentina (11),

8. Marekani (10),

9. Fiji (8),

10. Canada (7),

11. Uhispania (6),

12. Ireland (5),

13.Kenya (4),

14. Scotland (3),

15. Wales (2),

16. Japan (1).