Michezo

Afrika Kusini wajiondoa kwa kipute cha raga ya wanawake Botswana

May 15th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kuaibishwa mara mbili na Lionesses ya Kenya, miamba Afrika Kusini sasa wamejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Afrika cha raga ya wachezaji saba kila upande ya wanawake itakayoandaliwa nchini Botswana hapo Mei 26-27, 2018.

Lionesses, ambayo ilizaba Afrika Kusini 24-12 Aprili 5 katika mechi za Kundi X za kufuzu kushiriki Raga ya Dunia msimu 2018-2019 mjini Hong Kong na kuishinda tena 19-10 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia mnamo Aprili 14, sasa imeorodheshwa nambari moja katika orodha ya washiriki wataokuwa jijini Gaborone.

Kujiondoa kwa Afrika Kusini, ambayo ilipepeta Lionesses katika fainali za Kombe la Afrika mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017, kunawapa warembo wa kocha Kevin Wambua nafasi nzuri ya kushinda taji.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kuwazia kushinda taji, Lionesses lazima ipate matokeo mazuri katika Kundi A dhidi ya wapinzani wake Madagascar na Senegal. Kenya ilibwaga Madagascar 27-5 na Senegal 38-0 zilipokutana mara ya mwisho katika Kombe la Afrika nchini Tunisia mwezi Septemba mwaka 2017.

Kundi B linaleta pamoja mabingwa wa mwaka 2012 Tunisia pamoja na Uganda na Zimbabwe nao Morocco, Botswana, Mauritius na Zambia wako katika Kundi C.