Michezo

Afrika Kusini yaadhimisha mwongo mmoja tangu iwe mwenyeji wa Kombe la Dunia

June 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

AFRIKA Kusini inaadhimisha miaka 10 tangu iwe mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia katika soka ya wanaume mnamo 2010.

Licha ya kwamba timu za Afrika zimekuwa zikifanya vibaya katika mapambano hayo, zipo kumbukumbu nyingi za kutia moyo kutokana makala hayo ya 2010.

Mechi ya kwanza ya fainali hizo ilisakatwa Juni 11, 2010 uwanjani Soccer City jijini Johanesburg na iliwakutanisha wenyeji Afrika Kusini na Mexico.

“Ilitulazimu kujikakamua zaidi katika mchuano huo ili kuondoa dhana nyingi za kupotosha kwamba Afrika haikuwa na uwezo wa kuandaa fainali za haiba kubwa kiasi hicho na kwamba Waafrika ni watu wasioaminika,” akasema Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika Kusini (Safa), Danny Jordaan ambaye kwa wakati huo, alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kamati Andalizi ya Kombe la Dunia nchini mwao.

“Tulikuwa na presha nyingi ya kukabiliana na mitazamo hasi kutoka kwa mataifa mengi duniani, hasa yale tuliyowania pamoja tiketi ya kuwa waandalizi kisha yakaambulia pakavu. Yalikuwa yakitamani sana tufeli na fainali zenyewe ziwe za aibu kisha Afrika Kusini na bara zima lisalie kuwa kicheko,” akaongeza.

Nyota Siphiwe Tshabalala aliwafungia Afrika Kusini bao muhimu lililoduwaza dunia nzima mwanzoni mwa kipindi cha pili dhidi ya Mexico. Bao hilo ndilo limetazamwa zaidi kuliko yote kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia kupitia Youtube.

“Lilikuwa bao zuri lilinifanya kujihisi kwa namna ambavyo maneno yanakosa kuelezea. Goli hilo lilikuwa zawadi yangu kwa Afrika Kusini, bara zima na dunia yote,” akatanguliza Tshabalala.

“Ni tija na fahari tele kwamba hiyo ndiyo siku ambayo nyota yangu ilichaguliwa kung’aa. Nashukuru kuwa goli langu hilo, ambalo limesalia kumbukumbu, liliwaletea wengi furaha na kuwaunganisha mashabiki wa soka barani Afrika,” akasema.

Licha ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Mexico katika mechi ya kwanza ya makundi, kisha kupigwa na Uruguay na kusajili ushindi dhidi ya Ufaransa katika mechi ya mwisho, Afrika Kusini waliweka historia ya kuwa wenyeji wa kwanza wa fainali za Kombe la Dunia kushindwa kupiga hatua mbele baada ya mechi za raundi ya kwanza.

Kubanduliwa kwa Afrika Kusini kuliwasaza Ghana kuwa wawakilishi wa pekee wa bara la Afrika. Ghana almaarufu Black Stars waliweka historia ya kuwa timu ya tatu baada ya Cameroon mnamo 1990 na Senegal mnamo 2002 kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia kutoka Afrika.

Ghana walinyimwa nafasi ya kuingia nusu-fainali baada ya fowadi Luis Suarez wa Uruguay kutumia mikono kuzuia mpira kutikisa nyavu zao mwishoni mwa muda wa ziada kwenye robo-fainali. Suarez ambaye kwa sasa huvalia jezi za Barcelona, alionyeshwa kadi nyekundu na penalti ambayo Ghana walipewa ikapotezwa na mshambuliaji Asamaoh Gyan.

Tangu kuandaliwa kwa fainali hizo nchini Afrika Kusini, bara la Afrika liligeuka kuwa kivutio cha watalii baada ya miundo-msingi kuimarika, viwanja vya kifahari kujengwa, hoteli za haiba kupanuliwa, viwango vya soka kuboreka na mtazamo hasi wa awali kuhusu Waafrika kubadilika.

Ingawa hivyo, Jordaan ambaye pia ni Makamu Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), amesema yasikitisha kwamba fainali za Afrika Kusini hazitoa fursa maridhawa za mwamko mpya miongoni mwa mataifa ya humu barani hasa ikizingatiwa matokeo yao katika fainali mbili zilizofuatia; yaani 2014 nchini Brazil na 2018 nchini Urusi.

Mnamo 2014, Algeria na Nigeria zilifika raundi ya pili ya mwondoano huku wawakilishi wote watano wa bara la Afrika wakibanduliwa kwenye raundi ya kwanza mnamo 2018.

“Inatupasa kuanza kutathmini kiini cha kutofaulu kwa mataifa ya Afrika kwenye fainali hizi tangu Ghana ije pua na mdomo kuingia nusu-fainali,” akasema Jordaan.