Afya na Jamii

Afrika yabeba zigo zito la kisukari duniani

May 2nd, 2024 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

MTU mmoja kati ya watu 22 barani Afrika anaugua maradhi ya kisukari, na hii inawakilisha takriban watu milioni 24, mzigo mkubwa zaidi duniani.

Hii ndio ilikuwa mada ya majadiliano katika kongamano la kwanza kuhusu Mkakati wa PEN-Plus kuangazia maradhi yasiyoambukiza barani (ICPPA), jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kulingana na ripoti za utafiti, Afrika ya kati na sehemu za Kusini mwa Afrika ndizo zilizoathirika pakubwa zaidi.

Nchini Kenya, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), maradhi ya kisukari yameathiri asilimia 3.3 ya watu na kufikia mwaka wa 2025, inatarajiwa kwamba idadi hii itafika asilimia 4.5.

Wataalam wanasema kwamba hali hapa barani ni mbaya zaidi hasa ikizingatiwa kwamba watu wengi hawajui kwamba wanaugua maradhi haya.

“Hii ni kwa sababu baadhi ya visa hivi havitambuliwi hospitalini na kinaachochangia shida hii ni kwamba mifumo yetu ya afya hapa barani sio thabiti vilivyo kukabiliana na hali hii,” aeleza Dkt Santigie Sesay, Mkurugenzi wa idara ya maradhi yasiyo ya kuambukiza nchini Sierra Leone.

Katika harakati za kukabiliana na mzigo wa maradhi ya kisukari, mwaka wa 2021, WHO ilizindua mradi wa Global Diabetes Compact.

“Lengo lilikiwa kupunguza hatari ya ugonjwa wa kisukari na kuhakikisha kwamba watu wote wanaogundulika kuugua kisukari, wanafikia huduma bora ya matibabu,” aeleza Dkt Bianca Hemmingsen, Afisa wa Matibabu katika makao makuu ya WHO, nchini Uswisi.

Mojawapo ya sehemu za dharura zilizoangaziwa katika mradi huu ilikuwa kuongeza ufikiaji wa vifaa vya utambuzi na dawa za kukabiliana na maaradhi haya, na hasa insulini, katika mataifa maskini na yenye mapato wastani.

Lakini hii imeendelea kuwa changamoto barani huku utafiti ukionyesha kwamba bara la Afrika linavuta mkia katika ufikiaji wa bidhaa hii.

“Na ukosefu wa bidhaa hii ni mojawapo ya mambo ambayo yamefanya hali iwe ngumu zaidi barani,” aeleza Dkt Sesay.

Kulingana na utafiti wa WHO uliofanywa mwaka wa 2019, ni asilimia 36 pekee ya nchi barani Afrika zilioripoti kuwa na dawa muhimu za kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza.

Ni ripoti za aina hii ambazo zimechochea hatua kadha wa kadha kuchukuliwa na mataifa ya Afrika katika vita dhidi ya maradhi yasisyoambukiza.

Kwa mfano, mwaka wa 2022, mataifa 47 ya Afrika wanachama wa WHO barani, yalikubaliana kutekeleza mkakati wa PEN-Plus, katika mkutano ulioandaliwa nchini Togo.

Mkakati huu unanuia kuangazia mzigo wa maradhi yasiyosambaa hasa miongoni mwa wakazi wa maeneo ya mashambani, kupitia huduma katika vituo vya afya vya mashinani.