Afrika yajadili haja ya mfumo bora wa afya

Afrika yajadili haja ya mfumo bora wa afya

Na PAULINE ONGAJI

KUUNDA mfumo mpya thabiti wa kiafya ndio ujumbe uliotawala kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu afya ya umma (CPHIA 2021) juma lililopita, hafla iliyoandaliwa na Muungano wa Afrika (AU), na kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC).

Lakini mfumo thabiti wa Afya pia unahusisha huduma ya afya kwa watu wote (Universal health care), suala ambalo limekuwa changamoto kwa mataifa mengi barani. Huduma ya afya kwa watu wote (UHC) ilikuwa msingi wa mada ya majadiliano na Prof Francis Omaswa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afya ulimwenguni barani Afrika (ACHEST) na mwenyekiti wa taasisi ya usimamizi wa mifumo ya afya barani (Ashgovnet).

Umekuwa ukipigania sana suala la uwezo wa kila mmoja kufikia huduma nafuu za afya (UHC) barani Afrika. Sio wengi wanaoelewa hii ni nini. Hii inamaanisha uwezo wa nchi kutoa huduma za afya kwa kila mmoja kuambatana na uwezo wake wa kifedha. Hii inamaaisha kwamba kila nchi inapaswa kupanga huduma zake za afya kuhakikisha kwamba hata yule mtu wa chini hana ugumu wa kupokea matibabu.

Mataifa mengi ya Afrika, Kenya ikiwa miongoni mwao, hutegemea ufadhili kutoka nje ili kuendesha asilimia kubwa ya huduma za afya. Ndoto hii itatimiaje ikiwa mataifa ya Afrika yenyewe hayawezi mudu kujifadhili upande huu?

Kama nilivyosema UHC inahusisha nchi kutoa huduma za afya kuambatana na rasilimali zake za kifedha. Hii itaafikiwa iwapo mataifa ya Afrika yatatengea huduma za afya fedha zaidi. Kwa sasa mapendekezo ni kwa kila nchi kutumia angalau $ 86 kwa afya kwa kila mtu, lakini nchi nyingi za Afrika zinatumia pesa kidogo sana.

Ndoto hii itatimia kupitia ushirikiano na viongozi wa kisiasa kwani ni wao ndio wanaosimamia rasilimali. Ndiposa tunahitaji kikundi kingine cha watu kama vile wanahabari, vikundi vya kijamii na wanaharakati kujitokeza kuhakikisha kwamba pesa zaidi zinaelekezwa panapohitajika.

Wengi watauliza Kwa nini sasa? Ni jambo ambalo tumekuwa tukilizungumzia ila tu tumeibua gumzo hili tena. Mazungumzo haya yanaipa Afrika fursa ya mwanzo mpya kama ilivyokuwa wakati wa kujinyakulia uhuru. Wakati umewadia kwa bara hili kuziba pengo lililopo baina ya Afrika na sehemu zingine ulimwenguni katika masuala ya huduma za afya.

Kwa mfano kwa sasa Afrika inashuhudia ongezeko la idadi ya maambukizi ya maradhi ya COVID-19. Lakini hata tunapotoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati na kutupa msaada, tunapaswa kuelewa kwamba janga la mchipuko wa maradhi mapya litaendelea, na hivyo lazima mataifa ya Afrika yajiandae kwa uwezekano wa majanga ya aina hii katika siku zijazo.

Mradi wa UHC ni mojawapo ya maandalizi. Aidha, ni wakati wa nchi za Afrika kwa kuwa na uwezo wa kuunda, kuzalisha na kusambaza chanjo na vifaa vingine vya kimatibabu kwa ushirikiano na jamii ya kimataifa. Umetaja uongozi. Suala la uongozi mbaya limekuwa changamoto kwa baadhi ya mataifa ya Afrika. Ndoto hii itatimia vipi katika mazingira haya?

Suala la uongozi ni muhimu, na ndiposa Muungano wa Afrika umekuwa ukijitokeza waziwazi kukashifu mataifa yenye uongozi mbaya na yasiyo tekeleza demokrasia hapa barani.

Ili kuhakikisha kwamba wanasiasa wanawajibika, tunahitaji ushirikiano na wataalam kama madaktari kwani ni wao wanaojua mzigo wa kiafya miongoni mwa watu wa chini. Ningependa kutoa mwito kwa kwa wataalamu wa Kiafya barani kujitokeza , kushirikiana na kuwashurutisha viongozi ili wawajibike na kutengea huduma ya afya na matibabu, fedha kama inavyohitajika.

Mbali na suala la uongozi, nini kimezuia Afrika kutimiza ndoto ya afya kwa wote kwa muda huu wote?

Sababu ya kwanza kabisa ni umaskini ambao umelikumba bara hili kwa muda mrefu. Aidha, bara hili linakumbwa na tatizo la asilimia kubwa ya raia wake kuwa watu wachanga, kumaanisha kwamba hawawezi jitegemea. Huu ni mzigo mkubwa hasa kwa sekta ya afya.

Suluhisho ni nini? Suluhisho ni kuzungumza na viongozi wa nchi za Afrika na kuwarai kuwekeza zaidi sio tu katika afya, bali pia utafiti. Tatizo ni kwamba mataifa mengi ya Afrika huchukulia huduma ya afya kuwa mzigo, ilhali yaweza kuwa uwekezaji mkubwa. Sharti ujumbe huu ufikie viongozi wetu wa kisiasa. Hili litafanyika kupitia uhamasishaji.

Mashirika makuu barani yatasaidia vipi kuhakikisha ndoto hii inatimia ili haya yasiwe tu mazungumzo ya kawaida jinsi imeshuhudiwa awali? Tayari mashirika haya yamejitahidi ingawaje mengi yanahitajika kufanywa. Mfano mzuri ulikuwa kuundwa kwa Afrika CDC mwaka wa 2014, shirika ambalo limekuwana imekuwa likijitahidi kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba miradi ya huduma ya afya ya umma barani Afrika ni thabiti.

You can share this post!

Gharama ya maisha kero kuu kwa Wakenya-Ripoti

Makinda wang’arisha Arsenal Carabao Cup

T L