Michezo

Afriye na Ojwang watarajiwa kupatia Gor nguvu mpya CAF

September 11th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 18 na washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia wamepigwa jeki na marejeo ya masogora wawili wa haiba kubwa kambini mwao kadri wanavyojiandaa kwa mchuano wa Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League).

Chini ya kocha Steven Polack, Gor Mahia wanatarajiwa kuondoka humu nchini hapo kesho kuelekea Algeria kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa CAF utakaowakutanisha na USM Alger mnamo Jumapili.

Wanapojifua kwa kivumbi hicho, kambi ya Gor Mahia kwa sasa inatawaliwa na hamasa tele baada ya mvamizi Francis Afriye na beki Maurice Ojwang kuanza mazoezi kwa nia ya kuunga kikosi kitakachofunga safari ya kutua Algeria.

Akithibitisha hayo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Omondi Aduda amekiri kwamba Afriye na Ojwang watakuwa sehemu ya timu itakayotegemewa pakubwa na mkufunzi Steven Pollack dhidi ya USM Alger.

“Watakuwa katika kikosi kitakachosafiri. Tulikosa huduma zao katika mchuano wa raundi ya kwanza dhidi ya Aigle Noir ya Burundi. Kurejea kwao ni afueni tele kwa kikosi ambacho kinafahamu ugumu wa kibarua kilichopo mbele,” akasema Aduda.

Gor Mahia watakuwa wakipania kuweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza kutoka Kenya kuwahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi kwenye soka ya CAF.

“Tumekuwa tukibanduliwa mara kwa mara katika kivumbi cha CAF kwenye hatua za mwanzo. Nahisi kwamba kikosi kilichopo kwa sasa kina uwezo mkubwa wa kuboresha matokeo ya awali ya Gor Mahia,” akaongeza kinara huyo.

Gor Mahia walijikatia tiketi ya kuvaana na USM Alger baada ya kucharaza Aigle Noir kwa jumla ya mabao 5-1 yaliyopatikana katika mchuano wa mkondo wa pili uwanjani MISC Kasarani mwishoni mwa mwezi jana.

Kwa upande wao, USM Alger walifuzu baada ya kuwapokeza AS SONIDEP kutoka Niger kichapo cha 2-1 ugenini kisha 3-1 wakati wa marudiano.

Kufahamiana

Gor Mahia na USM Alger wanafahamiana sana baada ya kukabiliana katika mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) mnamo 2018. Gor Mahia walibanwa 0-0 jijini Nairobi katika mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kulemewa 2-1 nchini Algeria na hivyo kubanduliwa.

Inamaanisha kuwa Gor Mahia watakuwa wakitawaliwa na kiu ya kulipiza kisasi dhidi ya miamba hawa wa soka ya Algeria. Ingawa hivyo, ugumu wa kibarua cha Gor Mahia ni ubovu wa rekodi yao kila wanapocheza ugenini.

Mbali na Afriyie ambaye ni mzaliwa wa Ghana, Gor Mahia watalenga pia kutegemea zaidi maarifa ya mvamizi Nicholas Kipkirui na fowadi Gislein Yikpe Gnamian ambaye ni raia wa Ivory Coast. Watashuka dimbani wakitawaliwa na motisha ya kuwapepeta Tusker FC 5-2 katika mchuano wa kwanza wa kampeni za KPL msimu huu.