Habari Mseto

Afueni baada ya marufuku ya mifuko kusitishwa

April 4th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WATENGENEZAJI na wauzaji wa mifuko isiyoshonwa Alhamisi walijawa na furaha baada ya mahakama kuu kufutilia mbali agizo la Mamlaka ya Mazingira nchini (Nema) kuipiga marufuku.

Jaji James Makau alisimamisha marufuku ya Nema kwa wanaotumia mifuko hii akisema “haikushirikisha washika dau kabla ya kupinga matumizi yake.”

Jaji Makau aliamuru kesi iliyowasilishwa na wafanyabiashara wanaoiagiza mifuko hiyo kutoka ng’ambo isikizwe Mei 3, 2019.

Kesi ya kupinga hatua ya Nema iliwasilishwa mahakamani na wakili Kelvin Mogen (pichani juu) aliyemweleza Jaji Makau kuwa haki za wakenya zimekandamizwa na uamuzi huu wa Nema.

Aliomba mahakama ifutilie mbali agizo la Machi 31, 2019 la kuzuia wauazaji na waigizaji bidhaa hizi kutoka ng’ambo. Ombi lake lilisikizwa.

Pia korti ilizuia Nema kuwatisha watumiaji wa bidhaa hiyo.