Habari

Afueni baada ya kaunti zilizofungwa kufunguliwa

July 6th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Shughuli za kuingia na kutoka kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera zitarejelea hali ya kawaida mnamo Jumanne Julai, 2020.

Afueni hiyo imejiri zaidi ya miezi miwili baada ya kaunti hizo kufungwa, chini ya miongoni mwa mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kusambaa kwa homa ya corona.

Kwenye hotuba yake kwa taifa na iliyosubiriwa kwa hamu na wananchi kuona ikiwa atalegeza zaidi sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao wa Covid – 19, Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu alisema muda wa amri ya kuingia na kutoka nje ya kaunti hizo utakamilika kesho, Jumanne, saa kumi za asubuhi.

“Amri ya kuingia na kutoka nje ya Nairobi, Mombasa na Mandera inayoendelea kutekelezwa itafikia kikomo Jumanne, Julai 7, 2020 saa kumi za asubuhi,” Rais Kenyatta akatangaza.

Kiongozi huyo wa nchi hata hivyo alisema licha ya afueni hiyo, endapo hali ya maambukizi ya Covid – 19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, itageuka kuwa mbaya zaidi kwa kile alitaja kama “kuzidi kusafirisha ugonjwa huu kutoka eneo moja hadi lingine”, serikali haitakuwa na budi ila kutathmini uamuzi iliofanya.

Kwenye hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja kwa njia ya runinga kutoka Harambee House, Nairobi, Rais alisema ni jukumu la kila Mkenya kuchukua tahadhari kuzuia kusambaa kwa corona.

Taifa kuibuka mshindi dhidi ya Covid – 19, alisema ni jukumu binafsi la kila mmoja kujizuia kuambukizwa na pia kuzuia wanaomzingira, akieleza kwamba serikali imetekeleza wajibu wake.

Rais Kenyatta akionekana kushangazwa na shauku ya baadhi ya watu kwamba virusi vya corona havipo nchini, alisema: “Tusidanganyane huu ugonjwa hauko nasi. Huu ugonjwa uko nasi. Naskia wakisema si wa ukweli, si wa kushika au kuona. Idadi ya wanaoupata inaendelea kuongezeka. Jukumu la tahadhari liwe ni la kila mtu.”

Wafanyabiashara na wakulima, ni baadhi ya waliolalamikia kuathirika kwa amri ya kuingia na kutoka nje ya kaunti zilizofungwa.

Kufuatia kuendelea kwa hali ngumu ya maisha maeneo ya mijini, hasa jijini Nairobi, kutokana na athari za homa ya corona, wengi wanatarajiwa kuelekea mashambani kuanzia hii kesho.

Janga la Covid – 19, ambalo sasa ni kero la ulimwengu mzima, na linalotesa uchumi, limesababisha maelfu kupoteza nafasi za ajira, na baadhi ya biashara kufungwa, athari zinazochochea maisha kuwa magumu mijini.

“Kwa wale ambao wataenda nyumbani (akimaanisha mashambani), kwa nyanya au babu, baba au mama, jukumu la kuchukua tahadhari sasa si la serikali. Ikiwa utawapelekea ugonjwa, ile shida itatokea ujue wewe ndiye umewapelekea,” Rais Kenyatta akaonya, akieleza kwamba vita dhidi ya corona vitafanikiwa endapo wananchi watatumia mfano wa mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Kafyu ya kitaifa, na iliyoanza kutekelezwa Machi 27, 2020, imeongezewa muda wa siku 30 zaidi. Aidha, inatekelezwa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi asubuhi.

Maamuzi ya kufungua uchumi kwa awamu, Rais Kenyatta alisema yameafikiwa kwa ushirikiano na wataalamu wa sekta mbalimbali walioshauriwa, hata ingawa matakwa hitajika hayajatekelezwa kwa asilimia 100.