Habari Mseto

Afueni kwa Echesa na Matiang'i korti kuamuru wasilipe wasichana wa Pakistan

January 8th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Jumanne ilikataa kuamuru mawaziri wawili Rashid Echesa na Dkt Fred Matiang’i wawalipe Sh9 milioni wacheza densi wanane kutoka Pakistan waliofurushwa kutoka nchini Jumamosi kinyume cha maagizo ya mahakama.

Hata hivyo hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alimshauri wakili Evans Ondieki anayewatatea wasichana hao wanane na mmiliki wa kilabu cha Balle Balle kilichoko Parklands, Nairobi awasilishe ombi rasmi katika mahakama kuu ndipo suala la fidia hiyo isikizwe na kuamuliwa.

Na wakati huo huo Bw Cheruiyot alimpata Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) na hatia ya kukaidi agizo la mahakama kwamba awafikishe wasichana hao kortini jana (Jumanne) pamoja na mmiliki wa kilabu cha Balle Balle Bw Safendra Kumar Sonwani kortini.

Kiongozi wa mashtaka kutoka idara ya Uhamiaji Bw James Machirah alieleza mahakama kuwa wasichana hao wanane pamoja na Bw Sonwani wamefurushwa kutoka nchini Kenya.

“Wasichana hao wanane waliondolewa kwenye nyumba maalum inayomilikiwa na mwenye shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu ijulikanayo Blue Heart Bw Nadeem Khan na kurudishwa kwao Pakistan wasiendelee kuteseka na kuumia kimawazo,” alisema Bw Machirah.

Bw Machirah alimweleza hakimu kuwa hati zilizopewa wasichana hao kushiriki katika densi za kitamaduni Desemba 31, 2018 hazikuwa zimeidhinishwa na Bodi ya  Utalii (TRB) kabla ya kupewa visa na idara ya uhamiaji kukaa humu nchini hadi Januari 18, 2019.

Wasichana wa Pakistan washika kitambaa cha Blue Heart kabla ya kutimuliwa nchini. Picha/ Richard Munguti

Bw Machirah pia aliomba kesi dhidi ya wasichana hao na Bw Sonwani zitamatishwe kwa vile wamesafirishwa hadi Pakistan na India mtawalia.

“Kesi dhidi ya Bw Sonwani ilitegemea ushahidi wa wasichana hao na wamesafirishwa. Hakuna ushahidi. Naomba kesi zote mbili zifungwe,” Mr Machirah alisema.

Bw Sonwani na meneja wake Bw Mika Osicharo walikuwa washtakiwe kwa kesi ya ulanguzi wa binadamu kwa kuwaingiza nchini wasichana wanane kutoka Pakistan kinyume cha sheria mnamo Desemba 31, 2018.

Lakini mawakili Evans Ondieki na Dkt John Khaminwa walisema wasichana hawa walikuwa wamepewa vibali maalum na Waziri wa Utamaduni, Michezo na Jinsia Bw Rashid Echesa kushiriki katika densi za kitamaduni.

Mahakama ilifahamishwa kufurushwa kwa wasichana hao ni ukandamizaji wa haki zao na kuomba mawaziri Echesa na Matiang’i waadhibiwe.

“Maafisa hawa wa Serikali wamekaidi sheria za kimataifa ambapo Kenya ni mshirika kwa kuamuru wasichana hawa wanane wafurushwe kinyume cha maagizo yah ii mahakama,” walisema mawakili Khaminwa na Ondieki.

Waliomba Mabw Echesa na Dkt Matiang’i waadhibiwe kwa kuamriwa wawalipe fidia wasichana hawa ya Sh9 milioni kwa kukandamiza haki zao.

Akitoa uamuzi wake Bw Cheruiyot alisema, “Hii mahakama haitawaagiza mawaziri hawa walipe wasichana hawa fidia kabla ya maelezo kutolewa na DCI sababu aliwapeana walalamishi kwa idara nyingine ya Serikali.”

Kutoka kushoto: Mawakili Nadeem Khan, Evans Ondieki na mshukiwa Mika Osicharo wakiwa nje ya mahakama ya Milimani Januari 8, 2019. Picha/ Richard Munguti

Bw Cheruiyot aliwaamuru maafisa wawili wa uchunguzi wa jinai Mabw Samuel Ngunjiri na Julius Kiprotich wafike kortini Ijumaa kueleza sababu waliwapeana wasichana hao na Bw Sonwani kufurushwa nje .

Hakimu aliwataka wawili hao wawasilishe taarifa ya kiapo kueleza kilichojiri hata wakakaidi agizo la korti.

Bw Cheruiyot aliamuru Bw Osicharo aachiliwe kutoka seli za polisi kwa vile alikuwa mfanyakazi wa Bw Sonwani.

Awali Bw Machirah alieleza mahakama serikali imepanga jinsi ya kufanya na kilabu cha Bella Bella kinachokabiliwa na kesi kadhaa kuhusu ulanguzi wa watu . Mahakama ilimwuliza Bw Machirah sababu ya kutomwachilia Osicharo.

“Mbona unasema kuwa haki za wapikastani zimekiukwa na wameteseka kimoyo moyo. Je Osicharo ambaye alikuwa ameajiriwa na Sonwani hana haki za kukandamizwa,” hakimu alishangaa

Punde tu aliposema hayo aliamuru Osicharo aende nyumbani na kumweleza Bw Machirah , “suala hili la Echesa , Matiang’i na DCI halitakomea hapo.”

Bw Cheruiyot alimtaka Bw Ondieki awasilishe kesi dhidi ya maafisa hao wa Serikali waliokaidi maagizo yake.