Habari za Kaunti

Afueni kwa maskwota mahakama ikihimiza majadiliano na familia ya Kirima

January 18th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MAELFU ya wakazi katika shamba ambalo wanadaiwa walinyakua kutoka kwa familia ya aliyekuwa Mbunge wa Starehe Gerishon Kirima, wamepata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa kuamuru wafanye mashauriano.

Majaji Mohammed Warsame, Kairu Gatembu na Jessie Lesiit waliagiza ubomoaji usitekelezwe bali pande zote zishauriane.

Majaji hao waliamuru hali ilivyo sasa isivurugwe hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

“Baadhi ya masuala katika kesi hii yanatakiwa maelewano baina ya pande zote. Masuala hayo sio ya kuamuliwa na mahakama,” alisema Jaji Warsame.

Majaji hao waliamuru kesi hiyo itengewe muda kusikilizwa mapema iwezekanavyo.

Makundi mbalimbali yanadai umiliki wa shamba hilo.

Baadhi ya makundi hayo ni pamoja na Nardai Muoroto Self Help Group, Kamatuto Self-Help Group, na Queenspark Court-Tawala Owners Residents Association.

Familia ya Kirima aidha inadai ndiyo mmiliki halisi.

Mwaka 2023, Jaji Samson Okong’o aliwaamuru maswota wahame kwa shamba hilo.

Jaji huyo aliwataka maskwota hao wahame kufikia Desemba 31, 2023.

Lakini maskwota hao kupitia kwa wakili Francis Njanja walikata rufaa na kusitisha kutekelezwa kwa agizo la Jaji Okong’o kwamba wahame, wakidai walipewa na lililokuwa Baraza la Jiji la Nairobi ploti walizojenga ndani nyumba hizo.