Kimataifa

Afueni kwa mzee aliyefungwa kwa unajisi jaji kusema watoto ndio walimnajisi

February 7th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

JAJI wa mahakama moja ya Marekani alimpunguzia kifungo mzee wa miaka 67 ambaye alikuwa amehukumiwa gerezani kwa unajisi wa watoto wa miaka 13 na 14 na akasema kuwa watoto hao ndio walimnajisi mzee huyo.

Bw Raymond Soden alishtakiwa kuwanajisi watoto hao na akahukumiwa mwaka uliopita, lakini alipokata rufaa, Jaji Michael Gibbens alisema watoto hao hata si kuhusika katika kitendo hicho tu, bali walimvamia mzee huyo.

“Wadhulumiwa katika kesi hii walikuwa wavamizi hata kuliko wahusika katika tendo hili la jinai,” akasema Jaji Gibbens.

Alimpunguzia mzee huyo kifungo hadi miaka mitano na miezi kumi gerezani, kinyume na sheria ambayo inapendekeza kifungo cha chini kwa kosa hilo kuwa miaka 13.

Viongozi wa mashtaka tayari wameeleza kuwa wanapanga kukata rufaa, huku kikundi cha watetezi wa haki za binadamu kikipinga matamshi ya korti kuwa watoto hao ndio walikuwa wavamizi.

Jaji huyo alisema kuwa ni wasichana hao ambao walienda nyumbani kwa Soden na kwa hiari yao wakapokea pesa ili wafanye ngono naye.

“Hakika ni kuwa walikuwa wakiuza vitu ili walipwe pesa, hiyo ni kinyume na sheria hata kwa watu wazima,” akasema jaji huyo.

Lakini kiongozi wa shirika la Sunflower House Michelle Herman alisema kuwa kosa la dhuluma za kingono haliwezi kuwa hatia ya mdhulumiwa.

“Haijalishi kile wasichana walifanya ama hawakufanya, bado yeye (mshtakiwa) ndiye mtu mzima na hakuna yeyote anayefaa kufanyiwa hivyo,” akasema Herman.