Michezo

Afueni kwa Odoi kusamehewa katika kesi ya ubakaji

June 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Callum Hudson-Odoi wa Chelsea hataadhibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote kutokana na madai ya ubakaji yaliyotolewa dhidi yake.

Sogora huyo mzawa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 19 alitiwa mbaroni mnamo Mei 17, 2020 na kuachiliwa kwa dhamana.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, aliandika:

“Wakati ambapo mambo makubwa yanafanyika duniani kwa sasa, mtakumbuka pia kuhusu madai mazito yaliyowahi kutolewa dhidi yangu.”

“Nimesalia kimya tangu wakati huo na nimeshirikiana na kuwasaidia maafisa wa usalama katika kipindi chote cha uchunguzi wao kwa kuwa nilifahamu lilikuwa ni suala muda tu kabla ya ukweli kujulikana na jina langu kuondolewa kwenye orodha ya waovu.”

“Baada ya uchunguzi kamilifu na wa kina, polisi kwa sasa wamethibitisha kwamba hakuna hatua yoyote nyingine itakayochukuliwa dhidi yangu.”

Katika taarifa yao, polisi katika Kituo cha Metropolitan walisema: “Mwanamume aliyetiwa nguvuni mnamo Mei 17 kwa madai ya ubakaji ameachiliwa huru bila hatua yoyote kuchukuliwa dhidi yake. Hivyo, ina maana kwamba tukio alilohusishwa nalo kwa sasa halichunguzwi tena na polisi.”

Chelsea hawajatoa kauli yoyote kuhusiana na suala hilo.

Hudson-Odoi ambaye anajivunia kuwajibishwa na Uingereza mara tatu, alitia saini mkataba mpya wa miaka mitano na Chelsea mnamo Septemba 2019. Ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kupatikana na virusi vya homa kali ya corona.

Alipona na kurejea kambini kushiriki mazoezi ya pamoja na wanasoka wenzake kadri wanavyojiandaa kurejelea kampeni za EPL msimu huu kwa mechi itakayowakutanisha na Aston Villa ugenini mnamo Juni 21, 2020.

Hudson-Odoi aliongeza: “Ningependa kutumia jukwaa hili kumshukuru kila mmoja aliyesimama nami na kunitilia dua katika kipindi hiki kigumu.”

“Nimejifunza kwamba kuwa mwanasoka anayechezea mojawapo ya klabu bora zaidi duniani kufu ya Chelsea ni jukumu linalostahili uwajibikaji mkubwa. Kuanzia leo kwenda mbele, nitajitahidi kutumia fursa hii ya kuwa mchezaji wa Chelsea kuwa kielelezo chema kwa wenzangu kadri ya niwezavyo.”