Habari Mseto

Afueni kwa wafanyabiashara baada ya soko kufunguliwa

April 2nd, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUUZI wa kuuza vyakula katika Soko kuu la Madaraka , Makongeni, Thika wamepata afueni baada ya Soko hilo kufunguliwa tena baada ya kufungwa kwa muda wa wiki moja.

Wiki iliyopita soko kadha za kaunti ya Kiambu zilifungwa ili kukabiliana na homa kali ya Covid-19.

Baadhi ya Soko zilizofungwa ni ya Madaraka, Ruiru, na Githurai ili kunyunyizia dawa ya vieuzi (Sanitizer) na kuhamasisha wachuuzi hao jinsi ya kujikinga na homa hiyo bila kujumuika kwa pamoja.

Gavana wa kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alisema kila Soko litapulizwa dawa kabla ya kuruhusiwa kurejelea shughuli zake.

“Tulianza na soko la Madaraka, Makongeni, Thika, ambapo mnamo Jumanne Soko hilo liliweza kufunguliwa ili wananchi waendelee kununua vyakula. Hata hivyo wachuuzi walioko katika soko hiyo wamehimizwa kudumisha usafi wa hali ya juu kwa kunawa mikono na kuweka nafasi ya mbali kutoka kwa jirani wake,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema soko la Githurai na Ruiru zitafunguliwa baada ya kunyunyiziwa dawa.

Hata hivyo wachuuzi wa kuuza nguo za mitumba na viatu wameonywa kutoingia katika Soko hiyo kwa sababu vyakula havistahili kuwa mahali pamoja na nguo.

“Wachuuzi wa vyakula wanastahili kuwa pamoja peke yao bila kujumuka na wale wa kuuza nguo za mitumba. Hatutaki mchanganyiko kufanyika wakati kama huu,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema tayari kaunti ya Kiambu imeweka mikakati maalum kuona ya kwamba majiĀ  yamesambazwa kote katika Soko hizo ili kukabiliana na janga hilo la Corona.

Tayari Kampuni ya maji ya Thiwasco, na Bidco Africa Ltd, pamoja na washika dau kadha wamejitolea kununua mitungi ya maji na dawa ya vieuzi ili kukabiliana na homa hiyo.

Baadhi ya vituo muhimu vilivyowekwa mitungi ya maji ya kunawa ni hospitali, vituo vya magari, Soko, maofisini, na hata nje ya maduka katika mji wa Thika.

Hata hivyo ofisi nyingi za serikali zimefungwa, huku mikahawa,na maskani za pombe zikionekana mahame.

Mji wa Thika unaendelea kuwa na watu wachache baada ya bishara nyingi kufungwa. Biashara zinazoendelea kidogo ni matatu , bodaboda, na maduka machache za kuuza nguo na simu.