Habari Mseto

Afueni kwa wakazi wa Witeithie KWS ikinasa fisi wala watu

January 3rd, 2024 1 min read

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Witeithie, Juja wamepata afueni Mwaka Mpya 2024 baada ya Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) kuwanasa fisi wawili mnamo Desemba 31, 2023.

Maafisa wa KWS waliendesha operesheni kwa jina Ondoa Fisi Operation ambapo fisi hao walikamatwa na kurejeshwa katika mbunga za wanyamapori eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki.

Mnamo Novemba 2023, fisi waliwaua watu watatu–mwanamke na mwanamume kisha kijana aliyekuwa na umri wa miaka tisa.

Baada ya watatu hao kuuawa na fisi hao, wakazi wa eneo hilo walifanya msako wa kuwatafuta fisi ambapo waliwaua fisi wawili.

Walichukua hatua mkononi lakini haikusaidia kitu kwani inadaiwa fisi wengi wangali wanarandaranda katika maeneo ya matimbo ya mawe kijijini Witeithie eneo la Juja, na Kimincha.

Ilibidi viongozi kupaza sauti baada ya kutokea vifo vya wakazi hao ambapo walitoa wito kwa KWS kuingilia kati.

Mbunge wa Juja George Koimburi,  hapo awali alifanya mikutano na wakazi wa Juja na Witeithie ili kujadili kwa kina kuhusu usalama wa wakazi hao.

Kisa cha kwanza ni kwamba mwanamume mmoja alipatana na kundi la fisi usiku ambapo wanyama hao walimtafuna bila huruma.

Baadaye mwanamke mmoja alikuwa akielekea kazini majira ya alfajiri alipokumbana na kifo chake.

Naye kijana aliyekuwa na umri wa miaka tisa naye alitoka kanisani mwendo wa saa sita za mchana ambapo alizidiwa na wanyama hao wakamtafuna. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa karibu na eneo hilo wa kumuokoa.