Habari za Kitaifa

Afueni kwa Wakenya bei ya mafuta ikishuka zaidi

April 14th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MAMLAKA ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) imepunguza bei ya mafuta kwa hadi Sh18, kwenye bei mpya zitakazoanza kutekelezwa mwezi huu.

Kwenye taarifa Jumapili, Aprili 14, 2024, mamlaka hiyo ilisema kwamba bei ya petroli imepungua kwa Sh5.31 kwa lita, dizeli Sh10 kwa lita, huku mafuta taa yakipunguzwa kwa Sh18 kwa lita moja.

Kutokana na mabadiliko hayo, bei ya lita moja ya petroli jijini Nairobi itakuwa Sh193.84, dizeli Sh180.38, huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh170.06 kwa lita moja.

Jijini Mombasa, lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh190.66, dizeli Sh177.21, huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh166.99.

Jijini Nakuru, wakazi watanunua lita moja ya petroli kwa Sh192.90, dizeli Sh179.82, huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh169.56.

Bei hizo mpya zitatekelezwa kuanzia leo saa sita hadi Mei 14, 2024.

Wakenya waliozungumza na Taifa Dijitali walieleza kufurahishwa na bei hizo mpya, wakizitaja kama ishara ya gharama ya maisha kuanza kupungua.