Habari za Kitaifa

Afueni kwa Wakenya madaktari hatimaye wakiridhia kusitisha mgomo

May 8th, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI pamoja na Chama cha Madaktari na Wahudumu wa Afya hatimaye wameafikiana kusitisha mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya siku 56.

Maafikiano hayo yalijiri siku mbili baada ya Mahakama kuagiza kwamba pande zote kukubaliana kuhusu mfumo wa kurejea kazini lau sivyo iingilie kati na kutoa amri za kisheria.

Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa mwiba kwa muda mrefu ni malipo kwa matabibu wanagenzi ambao walilalamikia kupunguziwa mshahara kutoka Sh206,000 hadi Sh70,000 na kilichobainika ni kwamba suala hilo limebakia wazi bila utatuzi huku pande ya serikali ikisema kwamba utata wa malipo hayo upo kortini Eldoret na utashughulikiwa pindi uamuzi utakapotolewa.

Upande wa Chama cha Madaktari na Wahudumu wa Afya (KMPDU) nao unashikilia kwamba sharti wanagenzi hao watumwe kazini chini ya Makubaliano ya Pamoja ya 2017-21 ambao uliweka malipo yao kuwa Sh206,000.

Kwa mara kadhaa, Rais William Ruto amezungumzia suala hilo la mgomo, ikiwemo wakati wa sikukuu ya Leba Dei, akisema kwamba hakuna pesa za kuongezea mshahara madaktari kama walivyokuwa wanadai. Alisema ni sharti kuanza kuishi kwa kujimudu kama taifa akisisitiza kwamba Serikali inapambana kupunguza matumizi makubwa ya pesa aliyosema yametumbukiza nchi katika lindi la madeni.

Habari zaidi ni kadiri tunavyozipokea….