Afueni kwa wakimbizi

Afueni kwa wakimbizi

Na CHARLES WASONGA

WAKIMBIZI sasa wamepata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada unaowapa uhuru wa kuendelea kuishi nchini kwa kupata ajira na kuishi popote.

Kufutia hatua hiyo, zaidi ya wakimbizi 400,000 wanaoishi katika kambi ya za Dadaab na Kakuma sasa hawatarejeshwa kwao kwa nguvu jinsi serikali ilivyopanga kufanya miaka miwili iliyopita.

Kenya ilikuwa inapanga kufunga kambi ya Dadaab iliyoko Kaunti ya Garissa, na ile ya Kakuma iliyoko Kaunti ya Turkana kutokana na kile ilichosema ni “sababu za kiusalama.”

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i mnamo 2019 alitaja kambi hizo kama tishio kwa usalama nchini kwa kugeuzwa vituo vya wafuasi wa makundi ya kigaidi.

“Kambi za wakimbizi hazipaswi kusalia milele, zinafaa kuwa vituo vya muda. Tunawezaje kubeba mzigo huo kwa miaka 30? Wakati umewadia kwa kambi hizi kufungwa kwa sababu zimegeuka kuwa maficho ya magaidi,” Dkt Matiang’i akasema.

Lakini sasa kupitia kutiwa saini kwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Wakimbizi 2019 na Rais Kenyatta mnamo Alhamisi, serikali itasitisha mpango huo.

Chini ya sheria hii, wakimbizi sasa wataruhusiwa kusaka usaidizi wa mahakama za humu nchini endapo watahisi haki zao kuingiliwa.

“Mswada huo pia umefungua milango kwa wafadhili, yakiwemo mashiriki ya Umoja ya Mataifa (UN) kuelekeza pesa za kusaidia wakimbizi wanaoishi nchini Kenya. Kenya itapokea zaidi ya Sh4 bilioni kila mwaka kwa ajili ya mpango huu,” akasema Mbunge wa Homa Bay ambaye ni Mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama.

Kwa ujumla, Kenya inahifadhi zaidi ya wakimbizi 520,000 kutoka mataifa mbalimbali jirani. Wengi wanatoka Somalia, Sudan Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

You can share this post!

Chelsea wakomoa Leicester City na kupepea kileleni mwa...

Filamu ya ‘Monica’ ilichangia ajiunge na...

T L