Habari za Kitaifa

Afueni kwa wakulima wa kahawa serikali ikifuta madeni yao

June 11th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

BAADA ya presha kali kutoka kwa wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya kunakokuzwa kahawa kwa wingi, hatimaye serikali imefutilia mbali madeni ya kima cha Sh6.8 bilioni ambayo wakulima wa kahawa wanadaiwa nchini.

Uamuzi huo ulifikiwa Jumanne katika mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

“Katika mkutano huo, mawaziri walijadili na kuidhinisha kuondolewa kwa madeni ya Sh6.8 bilioni kwa wakulima wa kahawa na mageuzi mengine katika sekta ya kahawa,” ikasema taarifa iliyotumwa na Ikulu kwa vyombo vya habari baada ya mkutano huo.

Baraza la Mawaziri liliagiza vyama vya ushirika vya kahawa, vyama vya akiba na mikopo (saccos) na asasi nyingine zinazodai wakulima, kuwasilisha kwa Wizara ya Vyama vya Ushirika orodha ya wakulima wote wanaodaiwa na kiasi cha fedha.

Orodha hiyo itasilishwe kwa wizara hiyo ndani ya siku saba zijazo, ikiandamanishwa na stakabadhi zote zinazohitajika, kwa ukaguzi kisha malipo kwa vyama hivyo vya ushirika yatatayarishwa.

Hata hivyo, Baraza la Mawaziri lilionya kuwa madai yoyote ya uongo yatakayowasilishwa hayataruhusiwa.

“Visa vyovyote vya madai ya malipo ya uongo vitashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” taarifa hiyo ikasema.

Aidha, ili kuimarisha uzalishaji wa kahawa, mawaziri walisema kuwa Chama cha Ushirika cha New Kenya Planters Co-operative Union (New KPCU) kitaboreshwa zaidi ili kufikie viwango vya kimataifa.

“Vilevile, kushughulikia malalamishi kuhusu ubora wa kahawa, mitambo ya kisasa ya usindikaji wa kahawa itawekwa katika maeneo yote kunakokuzwa kahawa,” taarifa hiyo ya mawaziri ikasema.

Mawaziri walisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji wa kahawa hadi kiwango cha tani 200,000 kwa mwaka kufikia mwaka wa 2027.

Aidha, Baraza la Mawaziri lilisema kuwa mpango huo utajumuisha uimarishaji wa uzalishaji wa miche ya mikahawa chini ya Taasisi kuhusu Kahawa (CRI).

“Mpango huu utaifanya kahawa ya Kenya kununuliwa kwa wingi katika masoko ya kimataifa. Hali hii itaifanya sekta hii kuchangia maendeleo ya kitaifa kwa sababu zao hili ni mojawapo ya yale ambayo huiletea Kenya pesa nyingi yakiuzwa ng’ambo,” taarifa hiyo ikaendelea kueleza.

Katika siku za hivi karibuni, wanasiasa wa Mlima Kenya wamekuwa wakiishinikiza serikali kuondoa madeni wanayodaiwa wakulima wa kahawa ilivyo kwa wakulima wa miwa Magharibi mwa Kenya.