Afueni kwa wakulima wa mashamba madogo bima ya mimea ya bei nafuu ikizinduliwa

Afueni kwa wakulima wa mashamba madogo bima ya mimea ya bei nafuu ikizinduliwa

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kilimo na Kuangazia Mabadiliko ya Tabia Nchi Afrika (ACRE) limezindua mpango unaolenga kuangazia changamoto zinazozingira wakulima, kufuatia majanga ya mafuriko, ukame, wadudu waharibifu na magonjwa.

Mpango huo, The aMaizing Crop Insurance Programme, unapania kutoa bima ya mimea kwa wakulima wapatao 300, 000 wanaoendeleza shughuli za kilimo katika mashamba madogo ambao hawajafikiwa. Shirika hilo linatarajia kuwafikia kikamilifu kufikia Juni 2023.

Kulinganga na ACRE Africa chini ya huduma zake za bima, 2020 ilifanikiwa kusajili wakulima 128, 000 licha ya Kenya kukumbwa na janga la Covid-19. Kaunti 9 zinazojumuisha Nandi, Bungoma, Makueni, Machakos, Uasin-Gishu, Nakuru, Meru, Embu na Tharaka Nithi zimefikiwa kufikia sasa.

“Tunalenga wakulima wa mashamba madogo ili kuwapunguzia na hata kuwaondolea kero inayotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi (climate change),” Afisa Mkuu Mtendaji ACRE, Bw Ewan Wheeler akaambia Taifa Leo Dijitali katika mahojiano ya kipekee jijini Nairobi.

Akisisitiza kwamba shirika hilo limejitolea kwa hali na mali kuimarisha sekta ya kilimo nchini, Bw Wheeler alisema mbali na bima ya mimea, linashirikiana na kampuni zingine, hasa mashirika ya kifedha na pembejeo kutoa mikopo inayotozwa riba nafuu, mbegu, fatalaiza na dawa.

Afisa Mkuu Mtendaji Shirika la Kilimo na Kuangazia Mabadiliko ya Tabia Nchi Afrika (ACRE), Bw Ewan Wheeler…Picha/ SAMMY WAWERU

“Mpango wa bima, usambazaji mikopo na pembejeo, lengo lake ni kuhakikisha wakulima wanafidiwa majanga yanapojiri na kuongeza kiwango cha mazao,” akafafanua afisa huyo. Kupata huduma za ACRE unapaswa kuwa na simu ya kisasa ya tachi, unasaka apu ya mpango huo kupitia Google Play store kujisajili.

ACRE inasema ina apu kadhaa ilizoidhinisha, mahitaji kujiandikisha yakiwa maelezo yaliyoko kwenye kitambulisho cha kitaifa, shamba lilipo na aina ya mimea unayokuza kama mkulima. “Tulianza na DigiFarm, na kupitia kundi hilo wakulima wapatao 17, 400 wanaridhia huduma,” akadokeza Bw Amos Tabalia, Afisa Mkuu Msimamizi wa Utafiti na Maendeleo ACRE.

Alisema ada inayolipwa, ni wastani wa Sh700 ingawa kuna wakulima wanaolipa hadi Sh1, 500 kila msimu. “Mkulima anapopoteza mimea na mazao kupitia majanga anafidiwa kulingana na mikakati tuliyoweka,” Tabalia akasema.

“Kwa wasio na uwezo kimapato na wamejiandikisha, mashirika ya kifedha na pembejeo yanawakwamua kupitia mikopo na bidhaa za kulima.” Afisa huyo alisema mimea inayoendelea kuridhia bima ni mahindi, ngano, parsley, shayiri (barley), alizeti (sunflower), canola, maharagwe, viazi, ndengu, mpunga, kahawa na pamba.

Mkulima anaposhuhudia hasara, anafidiwa chini ya siku 7. Huduma zingine zinatolewa na ACRE ni matumizi ya mtandao wa picha, ambapo mkulima anatakiwa kupiga picha za mmea ulioathirika kutokana na magonjwa au wadudu anapakia kwenye apu kupata ushauri kutoka kwa wataalamu.

Vilevile, shirika hilo lina huduma za kupima kiwango cha maji kwenye udongo. ACRE inaendeleza mpango wa The aMaizing Crop Insurance Programme, kwa ushirikiano na Vandersat B.V na the Alliance of Bioversity International (CIAT), kupitia ufadhili wa pamoja na InsuResilience Solutions Fund (ISF).

Changamoto za wakulima kupoteza mimea na mazao kufuatia majanga ya mafuriko, ukame na mkurupuko wa magonjwa na wadudu zinaendelea kuwa kero kuu. Mabadiliko ya tabia nchi yanatajwa kuchangia changamoto hizo kwa kiwango kikuu.

Bw Amos Tabalia, Afisa Mkuu Msimamizi wa Utafiti na Maendeleo Shirika la Kilimo na Kuangazia Mabadiliko ya Tabia Nchi Afrika (ACRE)…Picha/ SAMMY WAWERU

You can share this post!

AFCON: Tunisia waponda Mauritania bila huruma katika Kundi F

AFCON: Sierra Leone walazimishia Ivory Coast sare ya 2-2...

T L