Habari Mseto

Afueni kwa wanougua kansa

November 15th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wagonjwa wa saratani watanufaika baada ya Hazina ya Matibabu kukusanya Sh100 milioni za kufadhili wagonjwa wasio na uwezo wa kugharamia matibabu maalum.

Hazina hiyo, Faraja Medical Fund, Jumatano ilisema itakuwa na uwezo wa kugharamia matibabu kama vile upasuaji, tibakemikali.

Kwa sasa, ugonjwa wa kansa husababisha vifo takriban 33,000 nchini kila mwaka huku wagonjwa wakizidi kuumia kutokana na ukosefu wa hospitali za kitaalam na wataalam wa kutibu ugonjwa huo.

Hazina hiyo ilipokea fedha hizo kutoka kwa wafadhili kwa lengo la kusaidia kulipia wagonjwa ambao hawana bima ya afya bili za hospitali.

Wanaohitaji wanafaa kutuma maombi kwa kujaza fomu maalum ili kutathminiwa na jopo maalum.

Watachagua atakayenufaika kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa aliyetuma maombi, umri, aina ya kansa na ubashiri wa kimatibabu.