Afueni kwa wavuvi kiwanda kikikamilika

Afueni kwa wavuvi kiwanda kikikamilika

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wavuvi 6,000 katika Kaunti ya Lamu wamepata afueni baada ya ujenzi wa kiwanda cha samaki eneo hilo kukamilika.Kiwanda hicho kilicho katika ofisi za Idara ya Uvuvi kisiwani Lamu kimegharimu kima cha Sh16 milioni na ujenzi wake umekuwa ukiendelea tangu 2019.

Ufadhili wake ulitoka kwa serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na shirika la masuala ya na mazingira na viumbe hai (WWF).

Akitangaza kukamilika kwa kiwanda hicho, Afisa Mshirikishi wa Idara ya Uvuvi, Kaunti ya Lamu, Bw Simon Komu, alisema mipangilio tayari inaendelea ili kukifungua rasmi kiwanda hicho mwezi ujao.Kiwanda hicho ni cha kipekee eneo hilo ambalo asilimia kubwa ya wakazi hutegemea uvuvi kujiendeleza kimaisha.

‘Madhumuni makuu ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni katika harakati za kupiga jeki sekta ya samaki na uboreshaji wa bidhaa hiyo,’ akasema Bw Komu.

Afisa wa WWF-Kenya, Bi Lily Dali Mwasi alisema shirika lake lilitumia zaidi ya Sh2 milioni katika ununuzi wa vifaa kama vile majokofu, mashini za kutengenezea samaki na uboreshaji wa bidhaa hiyo, mitambo ya moto unaotumia miale ya jua na vifaa vingine vingi.

Bi Mwasi alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuhifadhi na kutengeneza tani karibu 10 za samaki kwa wakati mmoja.Alisema furaha yake ni kuona wavuvi wa Lamu wakinufaika kwa kubadilisha hali yao ya maisha kupitia mradi huo.

“Tumeshirikiana na serikali ya kaunti ili kuutekeleza na kuukamilisha mradi huo wa kiwanda cha samaki. Natumai kuwepo kwa mradi huu kutasaidia kuinua maisha ya wakazi wa hapa hasa wavuvi,” akasema Bi Mwasi.

Mwenyekiti wa Makundi ya Uvuvi Lamu, Abubakar Twalib, aliipongeza serikali ya kaunti ya Lamu na WWF kwa kuwajengea kiwanda hicho cha samaki.

Bw Twalib alisema kwa miaka mingi, wavuvi wa Lamu wamekuwa wakikadiria hasara ya samaki wao kuwaozea na kuwatupa kutokana na ukosefu wa hifadhi na pia kiwanda cha kutengeneza samaki hao.Alisema kuwepo kwa kiwanda hicho ni mwanzo mpya kwao kwani wanatarajia pia kutaleta soko la samaki karibu na wavuvi.

“Tunafurahia kukamilika kwa kiwanda cha kwanza cha samaki eneo hili. Uwepo wake pia utapelekea samaki wetu kupata soko la haraka, jambo ambalo tumekuwa tukililia kwa muda mrefu,” akasema Bw Twalib.

Yusuf Ali ambaye ni mvuvi tajika kisiwani Lamu alisema kujengwa kwa kiwanda cha samaki, kaunti ya Lamu pia kutawaokoa kutokana ubahili wa madalali ambao wamekuwa wakiwanunulia samaki wao kwa bei ya chini.

You can share this post!

Uhuru na Raila wazindua miradi Nairobi na Kajiado

Uhuru na Ruto wajiuzulu ikiwa hawawezi kushirikiana –...