Afueni Mombasa kaunti ikirudishia vijana Kazi Mtaani

Afueni Mombasa kaunti ikirudishia vijana Kazi Mtaani

VIJANA wa Mombasa watapata afueni baada ya Bunge la Kaunti kupitisha mswada ambao utawapa vibarua vya kusafisha mazingiri ya mji huo.

Kwa mujibu wa madiwani wa wadi za kaunti hiyo, mpango huo wa kugatua ‘Kazi Mtaani’ utasaidia vijana wasiopungua 1,500 kupata riziki.

Mswada huo ulipitishwa wiki chache baada ya serikali ya kitaifa kusitisha mpango wa Kazi Mtaani, ulioanzishwa na serikali iliyoondoka majuzi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Utawala mpya wa Rais William Ruto uliamua kuwa vijana watahusishwa katika mpango mpya wa kupanda miti kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika mpango wa Kaunti ya Mombasa, vijana watakaoajiriwa kama vibarua watapewa jukumu la kusafisha mji huo wa kitalii hususan fuo za Bahari Hindi, kuondoa taka barabarani na mitaani na kwa jumla kudumisha mandhari ya kuvutia.

Hii inalenga pia kuridhisha maelfu ya wageni wanaotarajiwa kuzuru mji huo kwa likizo za Krismasi na Mpwaka Mpya mwezi wa Desemba.

“Janga la corona liliathiri uchumi wa Mombasa hasa baada ya kulemaza sekta ya utalii, ambayo ndio kitega uchumi cha Mombasa.

“Tunapokaribia msimu mkuu wa utalii mwezi ujao (Desemba), tunatumai utalii utanoga na wageni wengi kufurika Mombasa. Lakini taka zilizotapakaa zitawaudhi watalii, hivyo lazima ziondolewe,” akasema diwani wa Likoni, Bw Athman Mwamiri.

Diwani huyo aliomba pia vijana wapewe kazi ya uokoaji na upigaji mbizi katika fuo za Mombasa ili kutoa ulinzi kwa wageni wanaoogolea.

Yote tisa, mpango huo unanuia kuweka vijana bize badala yao kuzubaa na kuingiliea uhalifu mitaani.

Akizungumza katika mkutano wa usalama ulioitishwa na Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, Mbunge wa Jomvu Bw Badi Twalib alisema ukosefu wa ajira umechangia sana ongezeko la uhalifu mjini.

“Mipango kama hii ya Kazi Mtaani ni muhimu kuwapa vijana riziki. Ni lazima tuzuie uhalifu hususan msimu huu wa sherehe,” alieleza.

Kwa mujibu wa Gavana Nassir, vijana watakaoajiriwa katika mpango huo watasaidia kaunti kuwa safi huku wakijipatia riziki.

Aliahidi kushirikiana na viongozi wengine wa kaunti na kitaifa kukabili vilivyo ukosefu wa usalama.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama katika kaunti hiyo, Bw John Otieno, aliwahakikishia watalii kuwa usalama utadumishwa.

Mbali na ukosefu wa ajira, viongozi waliohudhuria mkutano huo walitaja pia uraibu wa dawa za kulevya kama unaochangia pakubwa visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.

Walimsihi Bw Otieno kuhakikisha maafisa zaidi wa usalama wanashika doria mara kwa mara wakiwa bila sare, hasa katika maeneo ambayo ni hatari.

Mbunge wa Kisauni, Bw Rashid Bedzimba, alisema kuwa eneobunge lake ambalo ndilo kubwa zaidi Mombasa likiwa na wadi saba, linakumbwa na ongezeko la visa vya utovu wa usalama katika wadi tatu.

Mitaa mingine ya kaunti hiyo ambayo hutajwa sana kama isiyo salama ni Mvita, Likoni na Nyali.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi wapepeta Qatar katika...

Wachungaji Thika wawatolea wito Wakenya waiunge mkono...

T L