Habari Mseto

Afueni Sukuma Bin Ongaro akijengewa nyumba

October 19th, 2020 2 min read

LEONARD ONYANGO na SHABAN MAKOKHA

GWIJI wa muziki wa benga Wilson Omutere, maarufu Sukuma Bin Ongaro, ni miongoni mwa maelfu ya Wakenya walioachwa bila makao kufuatia mafuriko yanayoendelea kusababisha hasara kote nchini.

Sukuma Bin Ongaro anaishi katika kingo za Mto Yala kijijini Ebukambuli Emutetemo, eneo la Mulwanda katika eneobunge la Khwisero, Kaunti ya Kakamega, na alikuwa miongoni mwa waathiriwa waliopoteza makao baada ya mto huo kuvunja kingo zake mnamo Machi, mwaka huu.

Mara baada ya mkasa huo, Bw Ongaro, 74, aliye na wake wawili na watoto 12, alitumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuomba Wakenya msaada.

Mnamo Mei, shirika lisilo la kiserikali, Aseka Miradi Foundation, lilijitokeza na kumpa msaada wa chakula na mabati 33 aliyotumia kujenga nyumba ndogo ya kujistiri.

Wanafunzi wa zamani wa shule ya msingi ya St Peter’s pia walijitokeza kumsaidia.

“Tuliposikia masaibu ya Bw Ongaro kupitia vyombo vya habari tuliamua kutumia kikundi chetu cha whatsapp kumchangia gwiji huyo wa muziki wa benga,” akasema Bw Bernard Washika ambaye ni msimamizi wa kikundi hicho.

Bw Washika alisema wanafunzi hao wa zamani wa St Peter’s waliunda kikundi hicho, kilicho na zaidi ya watu 200, ili kuchangiana fedha za kununua zawadi mmoja wao anaposherekea siku ya kuzaliwa.

“Baada ya kuchangisha fedha tulimtembelea msanii huyo nyumbani kwake na kuanza kujenga nyumba. Hatukutaka kuona mwanamuziki aliyevuma na kuwatumbuiza wengi akihangaika,” akasema Bw Washika.

Bw Ongaro jana Jumapili alisema kuwa alikuwa na furaha tele alipoona watu asiowajua wakimtembelea nyumbani kwake huku wakiwa na mafundi.

“Walipofika hapa walijitambulisha kwamba walikuwa wapenzi wa muziki wangu. Sikuamini waliponionyesha ramani ya nyumba waliyopanga kunijengea. Baadaye walianza kuchimba msingi,” akasema Bw Ongaro huku akisema kuwa Mungu amejibu maombi yake.

Kundi hilo linajenga nyumba itakayogharimu Sh1.8 milioni inayotarajiwa kukamilika Desemba 25. Kikundi hicho kitakongamana nyumbani kwa Bw Ongaro wakati wa sherehe ya Krismasi.

Nyumba hiyo ya vyumba vitatu vya kulala, ina vyoo viwili, jiko, chumba cha maakuli, stoo na sebule.

“Itakapokamilika tutaweka viti vya kisasa, mtungi wa gesi na televisheni ambapo atakuwa anafuatilia habari na kuburudika kwa muziki. Tunataka Bw Ongaro ajue kwamba angali anapendwa na kuheshimiwa,” akasema Bw Washika.

Bw Ongaro alisema kuwa ujenzi unaoendelea ni muujiza mkubwa.

“Nimekuwa nikisikia kwamba miujiza hutendeka lakini sijawahi kushuhudia. Lakini sasa nimejionea mwenyewe. Huu ni muujiza mkubwa, malaika wamekuja kunisaidia baada ya kupoteza mali yangu,” akasema Bw Ongaro.

Alisema mafuriko hayo yalimwacha akiwa maskini hohe hahe na hakuwa na uwezo wa kujenga nyumba nyingine.

Wahisani hao pia wanajenga bafu na choo cha shimo nyuma ya nyumba ya Bw Ongaro kwa ajili ya wageni ambao hawataweza kutumia vyoo vilivyo ndani ya nyumba.