Afueni wakazi wa Carwash-Zimmerman wakiimarishiwa barabara

Afueni wakazi wa Carwash-Zimmerman wakiimarishiwa barabara

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa eneo la Carwash lililoko Zimmerman, Nairobi wamepata afueni baada ya barabara ambayo imekuwa ikitatiza shughuli za usafiri na uchukuzi kuanza kukarabatiwa.

Barabara ya Rurii, inayounganisha Thika Superhighway na Kamiti Road imekuwa katika hali mbovu kwa zaidi ya miaka kumi.

Mvua ikinyesha hutatiza usafiri na uchukuzi kwa sababu barabara hiyo imekuwa na mashimo na mitaro hatari.

Shirika la Ustawishaji wa Jiji la Nairobi (NMS) limeanza kuboresha barabara hiyo.

Aidha, matingatinga yameanza kuilima, uongozi wa mradi wa wamiliki wa ploti ukidokeza kwamba itawekwa lami.

“Tumearifiwa NMS ina mipango ya kuiweka lami aina ya cabros,” mmoja wa viongozi Zimmerman Settlement Scheme na aliyeomba kutochapisha jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari akaambia Taifa Leo.

Agosti 2021, NMS kwa ushirikiana na Nairobi Water & Sewerage Company, ilianza kuimarisha miundomsingi ya majitaka, shughuli inayoendelea kutekelezwa.

Inachimba mitaro na kuweka paipu za kusafirisha majitaka.

“Kero kuu Zimmerman imekuwa majitaka kutapakaa kila mahali, kiasi cha kuathiri usambazaji wa maji. Tunaishukuru NMS kwa kuskia kilio chetu,” akasema Margaret Wanjiku, mmoja wa wamiliki wa ploti.

NMS ilizinduliwa mapema 2020 na Rais Uhuru Kenyatta, na kufikia sasa inaendelea kuboresha huduma za jiji la Nairobi, ikiwemo barabara, kuchimba visima vya maji na kuzindua vituo vya afya, kati ya miradi mingineyo.

Inaongozwa na Jenerali Mohamed Badi.

You can share this post!

Argentina na Paraguay waambulia sare tasa katika mechi ya...

Maoni mseto mitandaoni DCI ikianza kutumia Kiswahili...