Afueni ya bei ya mafuta yanukia Agosti

Afueni ya bei ya mafuta yanukia Agosti

JOHN MUTUA

HUENDA gharama ya maisha ikapungua kwa kiasi fulani kuanzia Agosti 2022 serikali itakapoanza kuagiza mafuta kwa bei nafuu kutoka Saudi Arabia kuliko bei ya sasa katika masoko ya ulimwengu.

Chini ya mpango huo Shirika la Kitaifa la Mafuta (NOC) litanunua petroli, dizeli, na mafuta taa moja kwa moja kutoka Shirika Saudi Aramco linalomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia.

Kampuni ya Aramco, inayomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia imetajwa kuwa kubwa zaidi duniania na huu mafuta katika masoko ya mabara ya Asia, Uropa na Amerika Kaskazini.

“Tayari tumetia saini mkataba wa maelewano (MOU) na hatua itakayofuata ni kujadili masharti ya kandarasi wakati wowote kuanzia sasa, “ Afisa Mkuu Msimamizi wa NOCK Leparan Ole Morintat alisema Jumatatu.

Chini ya MOU hiyo shirika la Nock litaagiza asilimia 30 ya mahitaji ya mafuta nchini kuanzia Agosti mwaka huu, hali ambayo inaweza kuchangia kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo na kutoa afueni kwa Wakenya.

Hata hivyo, muda wa utekelezaji wa mkataba huo ambao unasimamiwa na serikali mbili za Kenya na Saudi Arabia, haujulikani.

Chini ya maelewano hayo, shirika la Saudi Aramco ndilo litagharamia usafirishaji wa mafuta hadi nchini Kenya. Aidha, litaliuzia Nock mafuta kwa mkopo ambao utalipwa ndani ya siku sitini (60) au siku tisini (90).

Isitoshe, chini ya mpango huo, serikali ya Kenya itaweza kuagiza mafuta ya akiba ya kimkakati kuikinga nchi kutokana uhaba wa mafuta endepo usambazaji wa bidhaa katika soko la kimataifa utavurugwa.

Uchumi wa Kenya umeathirika na kupanda kwa bei ya mafuta kwa kiwango cha juu kupita kiasi huku petrol ikiuzwa kwa Sh159.12 kwa lita moja jijini Nairobi. Dizeli inauzwa kwa Sh140 kwa lita huku mafuta taa ikiuzwa kwa Sh127,94 kwa lita.

Hali hii imechangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi katika masoko ya kimataifa kufuata vita vinavyoendelea kati ya mataifa ya Urusi na Ukraine.

Hatua ya Urusi kuvamia Ukraine mnamo Februari 24 mwaka huu ulichangia mataifa ya ulimwengu kuiwekea nchini hiyo vikwazo vya kibiashara. Vikwazo hivyo vimeizuia Urusi, ambayo ndio ya tatu katika uuzaji wa mafuta ulimwenguni, kuuza mafuta yake katika masoko ya ng’ambo.

Hali hiyo imechangia Kenya kulazimika kununua mafuta kwa bei ya juu kutoka mataifa mengine kwa sababu shirika la Nock huwa haliweki mafuta ya akiba kukidhi mahitaji ya kitaifa nyakati za uhaba.

Shirika la Nock ambalo lilibuniwa kwa lengo la kusimamia bei ya mafuta limeshindwa kutekeleza wajibu huo kutokana na ushindani kutoka kwa kampuni za kibinafsi za mafuta.

Awali, lilinuiwa kuagiza asilimia 30 ya hitaji la bidhaa za mafuta, ikiwemo gesi ya kupikia lakini lilishindwa kutekeleza wajibu huo serikali ilipotoa nafasi kwa kampuni za kibinafsi za mafuta kuagiza bidhaa hiyo.

Kampuni hizo ni kama vile Vivo Energy Kenya, TotalEnergies na Rubis Energy. Wakati huu, Nock huagiza asilimia 2.2 pekee na mahitaji ya mafuta nchini huku Vivo Energy Kenya ikiagiza asilimia 26.52, TotalEnergies (asilimia 17.7) na Rubis Enegry (asilimia 10.73).

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Urusi yalemewa kulipa madeni yake ya kigeni

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa MS hauna tiba lakini waweza...

T L