Lugha, Fasihi na Elimu

Afueni yaja Machogu akizitaka shule kupunguza karo

April 22nd, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

KARIBU wiki moja kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula wa pili, serikali sasa inataka wamiliki wa taasisi za elimu za kibinafsi kupunguza karo za shule.

Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, alikosoa gharama ya juu ya shule za kibinafsi akiwataka wamiliki wa shule hizo kupunguza karo ili kuwezesha wanafunzi wengi kupata elimu bora.

Shule za msingi za kibinafsi hutoza karo kati ya Sh15,000 hadi Sh100,000 na kuendelea.

Watoto katika shule hizo, tofauti na wenzao katika shule za umma ambao hawalipi ada ya masomo, huwa wanafurahia elimu bora, lugha za kigeni, shughuli za ziada kama vile kuogelea, miongoni mwa michezo mingine.

Bw Machogu alitaja Chama cha Shule za Kibinafsi cha Kenya kama mshirika wa thamani katika harakati za kutoa elimu bora kwa kila mtoto nchini Kenya.

Alisema kwa kuendeleza mazungumzo ya wazi, kufanya kazi kwa ushirikiano, na kutafuta masuluhisho ya kiubunifu, wanaweza kuunda mfumo ikolojia wa elimu ambao ni bora, endelevu na unaojumuisha wote.

“Ndio maana nawasihi mshirikiane na serikali kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa shule za kibinafsi na kufanya elimu bora ipatikane kwa wote,” alisema waziri huyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Elimu wa eneo la Pwani, Lucas Kangongo.

Mwenyekiti wa Chama cha Shule za Kibinafsi nchini (KPSA), Charles Ochome, alisema wadau hao watashirikiana na serikali kuimarisha masomo.

“Tunatoza ada za shule kulingana na gharama za uendeshaji. Iwapo serikali inaweza kupunguza gharama za uendeshaji itapunguza moja kwa moja karo za shule,” alisema.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Shule za Kibinafsi (KPSA) mnamo Ijumaa, Waziri huyo aliwapongeza washikadau hao kwa kutoa elimu bora.

“Imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio mengi tuliyoyapata katika sekta hii. Tunatambua haja ya kuziba pengo hilo na kuhakikisha masuala ya ufanisi, umuhimu, ubora, ufikiaji na usawa yanashughulikiwa,” alisema waziri.

Alisema Serikali imeshirikiana kwa karibu na chama hicho kuhakikisha sera ya mpito ya asilimia 100 kutoka elimu ya msingi hadi sekondari inafanikiwa.