Kimataifa

Afueni yanukia kwa Jumwa baada ya kulala ndani siku 7

October 26th, 2020 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa anatarajiwa kurejea nyumbani leo baada ya kulala katika seli za Kituo cha Polisi cha Bandarini kwa siku saba.

Wakili wake, Bw Cliff Ombeta jana aliambia Taifa Leo kwamba hata baada ya mteja wake kupewa dhamana mnamo Ijumaa, hangeweza kutoka kwa kuwa muda ulikuwa umeyoyoma.

“Tulikuwa na pesa taslimu lakini tulipata nakala ya uamuzi wa mahakama kuchelewa. Lakini tutawalipia leo asubuhi na watakuwa huru,” akasema Bw Ombeta kwa njia ya simu akimrejelea mbunge huyo na mlinzi wake Bw Geoffrey Okuto.

Bi Jumwa na Bw Okuto hadi jana walikuwa wamesota korokoroni kwa siku saba mfululizo tangu kuwasilishwa kortini kuhusiana na mauaji ya Bw Ngumbao Jola.

Bi Jumwa alitakiwa kuwasilisha dhamana ya Sh 3 milioni au kulipa pesa taslimu Sh4 milioni ili kupata uhuru wake. Naye Okuto kwa upande wake alitakiwa kupata dhamana ya Sh1 milioni au kulipa pesa taslimu Sh1.5 milioni kabla ya kuachiliwa.

Jaji wa Mahakama ya Juu Njoki Mwangi aliwapa dhamana hiyo baada ya kupuzilia mbali ombi la upande wa mashtaka la kuwataka wawili hao wazuiliwe hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa. Jaji huyo alisema kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha sababu za kutosha za kuwezesha mahakama kuwanyima washukiwa hao dhamana.

Jaji Mwangi alitegemea ripoti ya afisa mdadisi, ambayo ilionyesha kuwa washukiwa hao wanaweza kupatikana hata wakiachiliwa kwa dhamana.

Vilevile, pendekezo la chifu wa eneo analoishi Bi Jumwa lilichangia pakubwa kuachiliwa kwake kwa dhamana, kwani lilionyesha kuwa hakuna uwezekano wa fujo kutokea akiwa huru.

“Mshukiwa amekuwa akifanya harambee na kutangamana na wananchi katika eneo hili na hakujawahi kushuhidiwa fujo. Si Kweli kuwa kuachiliwa kwake kutaleta hatari,” alisema chifu wa eneo la Ganda, Bw Batholomew Kitunga.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa Bi Jumwa na Bw Okuto wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa miaka sita iliyopita.

“Uchunguzi ulithibitisha kuwa Bi Jumwa aliachana na mumewe wa kwanza zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kwa miaka sita iliyopita, amekuwa katika uhusiano thabiti na Bw Okuto, ambaye ni mshtakiwa mwenzake katika kesi hii,” ilisema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa Bw Okuto ameoa na kuwa ana watoto wawili. Mahakama iliambiwa kuwa madai ya kuwa alitengana na mkewe, ambaye alimuoa mnamo 2009 si ya ukweli.

Pia, mahakama iliambiwa kuwa mke wa Bw Okuto anajua ukweli kwamba mumewe aliajiriwa na Bi Jumwa kama msaidizi wake wa kibinafsi, kabla ya uhusiano wao wa kimapenzi kunoga.

Akiwa Malindi, polisi wanasema Bw Okuto hukaa nyumbani kwa Bi Jumwa na wakiwa Nairobi, anakaa Lavington. Amekuwa akiishi pamoja na mbunge huyo kwa miaka sita sasa.