Habari

'Afufuka' kabla ya kuzikwa

August 5th, 2019 2 min read

NA GEORGE ODIWUOR

KIJIJI cha Godmiaha, eneo la Rachuonyo Mashariki, Kaunti ya Homa Bay kiligeuka uwanja wa kioja Jumamosi wakati mwanamume ambaye mazishi yake yalikuwa yakiendelea alipoingia kwenye boma na kusimama mbele ya waombolezaji akiwa buheri wa afya.

Wanakijiji walibaki midomo wazi wakistaajabu jinsi Bw Kennedy Olwa wa umri wa miaka 38, ambaye walidhani mwili wake ndio uliokuwa ndani ya jeneza tayari kuzikwa, alivyojitokeza mbele yao, wengine wakidhani amefufuka.

Bw Olwa aliondoka nyumbani zaidi ya miaka 20 iliyopita na kuelekea mjini Mbita, ambako alifanya kazi ya uvuvi kabla ya kuhamia ufuo wa Alum katika Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kaskazini.

Muda huo wote wa miaka 20 hakuwa ameenda nyumbani kwa wazazi wake.

Kulingana na Chifu wa Lokesheni ya Ramba, Bw Joseph Ndege, familia ya Bw Olwa ilipata habari kwamba alikuwa amefariki baada ya kuugua, na mwili wake ukapelekwa na maafisa wa polisi katika mochari ya Hospitali ya Kaunti ya Homa Bay.

“Baada ya kupata habari hizo, familia ilianzisha mipango ya mazishi mara moja. Baadhi ya jamaa zake waliotumwa katika mochari walithibitisha mwili huo ulikuwa wa Bw Olwa,” akasema Bw Ndege.

Familia ilienda hatua moja zaidi na kutangaza kifo chake katika redio kisha ikatumia kiasi kikubwa cha pesa kununua vyakula vya kuwalisha waombolezaji, na kufanikisha mipango mingine ya mazishi.

Cha kustaajabisha ni kwamba wakati huo wote Bw Olwa alikuwa akisikiza kifo chake kikitangazwa redioni alipokuwa akiendesha shughuli zake kwenye ufuo wa Alum.

Pia ilifahamika kuwa aliwasiliana na baadhi ya wanakijiji aliowafahamu na kuwaarifu kwamba angali hai. Lakini hakuna aliyeamini wakidhani ni mtu mwingine aliyekuwa akiwachezea, ndiposa wakaendelea na maandalizi ya mazishi.

“Alipiga simu kwa baadhi ya jamaa zake nyumbani na kuwashauri kusitisha mipango ya mazishi. Familia pia iliwatuma jamaa wengine hadi ufuo huo ili kuthibitisha kama bado alikuwa hai au la baada ya kupata habari kuwa alikuwa akisema yupo hai,” akasema Bw Ndege.

Hata hivyo familia haikuamini bado alikuwa hai kwa kuwa hawakuwa wamezungumza naye kwa miaka 20.

Walichukua mwili walioambiwa ni wa jamaa yao kutoka mochari mnamo Ijumaa iliyopita, na Jumamosi mchana walikuwa tayari “kumzika” Bw Olwa bila kufahamu alikuwa hai.

Ukweli ulibainika wakati kikundi cha jamaa wa familia waliotumwa ufuoni Alum waliporudi Jumamosi wakiwa wameandamana na Bw Olwa.

Huku jamaa waliokuwa mazishini wakistaajabishwa na mwenzao aliyekuwa hai, wale ambao waliwasili na Bw Olwa walipigwa na butwaa kupata kwamba ibada ya mazishi yake ilikuwa ikiendelea baada ya ‘mwili’ wake kuletwa nyumbani Ijumaa.

Hafla hiyo ya mazishi ilitibuka baada ya Bw Olwa kuwahakikishia jamaa kwamba yupo hai na mwili uliodhaniwa kuwa wake ukarejeshwa hospitali ya Kaunti ya Homa Bay.