Makala

Afunguka jinsi maisha yalimtesa, mama yake akiolewa na wanaume 10 tofauti

October 28th, 2020 4 min read

Na SAMMY WAWERU

Nicholas Muturi ni mwingi wa tabasamu, furaha na bashasha unapopata fursa ya kutangamana naye.

Ni mkwasi wa ushauri na nasaha hasa kwa wanafunzi na vijana kwa jumla, ujumbe ukiwa; “Licha ya magumu au mazito unayopitia ama kukumbana nayo, Mungu yupo na ipo siku atarejesha tabasamu yako.”

Ni hulka ambazo zimeficha mengi ambayo Nicholas Muturi amepitia, ila sasa ana kila sababu ya kutabasamu na kuwa kielelezo katika jamii.

Yeye pamoja na dadake mdogo, mzawa, ni mayatima, na Muturi anaungama “Mungu ndiye mama na baba wa wasio na wazazi”.

Alizaliwa mnamo Aprili 24, 1992, katika Kaunti ya Kirinyaga, mwaka anaosema kwamba mamake alikuwa angali mdogo sana kiumri. “Alinizaa akiwa na umri mdogo mno, miaka 14,” anasema.

Anafichua, alikuwa katika darasa la saba wakati huo, na alilazimika kuacha masomo, ili kuitika wito wa majukumu ya ulezi.

Hata ingawa kufikia sasa kutambua au kujua babake mzawa imekuwa kitendawili kilichokosa mteguzi, Muturi anasema mamake hakuwa na budi ila kuolekea aliyemtunga ujauzito, yaani babake.

Hata hivyo, Muturi anasimulia kwamba ndoa hiyo haikudumu kwa kile anataja kama “baba kushindwa kutukithi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi”.

Hatimaye, hakuwa na budi ila kurejea nyumbani, na kwa mujibu wa simulizi yake wakati huo Muturi alikuwa na umri wa miezi kadhaa pekee.

“Baadaye mama aliolewa kwa mwanamume mwingine, ambaye ni baba mzazi wa dadangu. Ndoa hiyo ilidumu muda wa miaka mitatu pekee,” anafichua, akisema wakati wa wawili hao kuachana alikuwa na miaka minne na nusu.

Kulingana na Muturi, utengano huo kwa kiasi fulani uilikuwa wenye sarakasi na drama.

Anasema kilichoanza kama mzaha, mama kutorejea nyumbani siku na wiki kadhaa kwa sababu ambazo hazikiueleweka, kiliishia baba yao kuwapeleka kwa kina nyanya, mama aliyezaa mama yao.

Nicholas Muturi, kijana mkakavu na mcha Mungu aliyepitia mengi maishani. PICHA/ SAMMY WAWERU

Siku iliyofuata, anasema nyanya aliwarejesha kwa baba yao tena, ikawa kana kwamba “wanarushiana watoto”.

Hatimaye, nyanya hakuwa na budi ila kuwaitikia baada ya baba yao kuwarejesha tena, na mara hiyo kuwaacha nyuma ya nyumba ya nyanya usiku. “Kwa huruma, nyanya alituchukua na siku chache baadaye, mama alitujia ambapo tayari alikuwa katika ndoa nyingine, baba wa tatu,” anaelezea.

Baba wa tatu, anamtaja kama “Baba wa ajabu”. “Mchana alikuwa mhudumu wa buchari, na usiku alishiriki uhalifu. Ninakumbuka, nikiwa darasa la pili alikamatwa baada ya kushiriki wizi, na alipofikishwa kortini na kushtakiwa akapatikana na hatia ambapo alihukumiwa kuhudumu kifungo kirefu cha jela,” anafichua.

Ni hatua ambayo ililazimu mamake kuwarejesha kwa nyanya tena, kwa sababu hakuweza kumudu kuwakimu riziki.

Muturi anaendelea kueleza kwamba, maisha humo hayakuwa rahisi. Walilazimika kulalia tandiko la gunia, kwa kuwa mamake asingemudu kununua kitanda na godoro. Ilikuwa hali ngumu kwa watoto wenye umri mdogo, Muturi akidokeza kwamba waliugua Homa mara kwa mara.

“Ndoa iliyofuata, ilikuwa ya mwanaume aliyeonekana kuwa nadhifu, ila iliishia kuwa ya dhuluma kwa dadangu bila ufahamu wa mama. Nikiwa darasa la tano, waliachana,” Muturi anasema.

Ni matukio yaliyoendelea kwa muda, akikadiria kina baba aliopitia mikononi mwao ni zaidi ya 10, watatu kati yao wakiuawa kwa sababu ya kushiriki uhalifu.

Aidha, ni kutokana na maisha magumu Muturi na dadake walipitia, aliamua kukaza kamba masomoni. Nyakati zingine, wawili hao walilala njaa.

Huenda mamake barobaro huyu alichohitaji ni kuwa na familia kamilifu, yaani yenye baba na mama, ili watoto wawe na kielelezo lakini ndoto zake hazikuafikika.

Licha ya magumu maishani aliyopitia, ikiwemo kukosa chakula na karo kukata kiu cha masomo, ameibuka kuwa mshindi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Kulingana na Mwinjilisti Janet Esther, ambaye ni mshauri nasaha wa masuala ya ndoa, hakuna kitu muhimu katika malezi ya mtoto ama watoto, kama kuona wana kielelezo cha baba na mama.

“Kwa hakika, ni wachache mno wanaoridhia maisha ya singo fatha au singo matha. Ni matamanio ya mzazi kuona watoto wana mama na baba, ambao ni kioo katika jamii,” Mwinjilisti Janet anaelezea.

Kulingana na mtaalamu huyo, si rahisi kushawishi mtoto, hasa kumweleza kwa nini baba au mama hayupo. “Watoto wanapotangamana shuleni, husifia wazazi wao, mfano ‘utaskia mmoja akisema alicholetewa na baba au mama, ama ahadi alizopewa ikiwa atafanya vyema kwenye mtihani’,” anafafanua.

Huku watoto hao wakiendelea kupitia machungu, Muturi anasema alichokosa maishani ni “mwanamume ambaye angekumbatia kama baba”.

Licha ya lindi hilo la mazito aliyopitia, alitia bidii masomoni. Mwaka wa 2005 alifanya mtihani wa kitaifa darasa la nane, KCPE na kupata alama 313 kwa jumla ya 500, zinazowezekana.

Hata hivyo, mamake aliyetegemea vibarua vya hapa na pale, na ambavyo nyakati zingine vingekosekana, hakuwa na uwezo kumlipia karo kujiunga na shule ya upili.

Isitoshe, nyanya aliugua na familia ambayo angeitegemea kumpiga jeki kimasomo, ilijikakamua kuokoa maisha ya nyanya.

Muturi anasema hakuwa na budi ila kurudia darasa la nane, ambapo mwaka mmoja baadaye alipata alama 365. Mwaka huohuo, 2006, ndio nyanya aliaga dunia.

“Mambo hayakuwa rahisi, mara nyingi nilikosa chakula cha mchana ila matumaini yangu niliyaelekeza kwa Mwenyezi Mungu,” anasimulia.

Anasema licha ya kufanya bora katika KCPE awamu ya pili, hakukuwa na pesa kumuwezesha kujiunga na shule ya upili.

Alikawia kujiunga na kidato cha kwanza, na ni kupitia ukodeshaji wa kipande cha shamba mamake alikuwa amepewa alifanikiwa kuingia shule ya upili. Muturi anasema masomo yake yalifadhiliwa kupitia mgao wa Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF).

Kiu cha kupata elimu, hakikukatizwa na changamoto chungu nzima alizopitia. “Kidato cha nne, nilifanya KCSE mwaka wa 2010 nikazoa B- na kwa sababu matokeo hayo yasingeniwezesha kujiunga na orodha ya wanaofadhiliwa na serikali kiwango fulani cha karo, niliamua kurudia, kupitia ufadhili wa bodi ya shule nilyosomea,” anaelezea.

Jaribio la pili 2011, Muturi anasema alizoa alama ya B+, na ambapo 2012 alipata nafasi kujiunga na Chuo Kikuu cha Masuala ya Sayansi na Teknolojia Meru, akasomea Shahada ya Hisabati, Kompyuta na Sayansi.

Anasema masomo yalifadhaliwa na wanajamii na walimu wa shule ya upili aliyosomea.

“Wakati huo mama alifanya kazi kama mhudumu wa baa. Nikiwa mwaka wa kwanza chuoni, alipatikana na Saratani, akalazimika kuacha kazi, akaingilia vibarua vya kuchuhuma majanichai,” anadokeza, akisema ni hatua iliyomlazimu kuacha masomo mwishoni mwa mwaka wa pili chuoni, ili kumtunza, hali yake kiafya ilipoanza kudhoofika.

Kijana huyu anasema akiwa chuoni, mamake alikuwa wa msaada mkuu. Hata hivyo, Desemba 2014, alifariki, Muturi na dadake wakaachwa watoto yatima. Aliaga dunia mwaka ambao dadake alifanya KCSE, na kuzoa alama B-.

“Tumeng’ang’ana, na kufikia tulipo ni kwa neema za Mungu,” anaeleza barobaro huyo mcha Mola.

Muturi kwa sasa ni mwalimu wa shule ya upili ya kibinafsi ya St. Joan’s Murang’a Girls. Isitoshe, anasema ni mwanachama wa Shirikisho la Kitaifa la Kikristo la Wanafunzi (KSCF), linalotoa mafunzo ya nasaha na ushauri kwa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.

Barobaro huyu anayehimiza wazazi kupenda watoto wao, licha ya pandashuka wanazopitia, ametunga vitabu vyenye mafunzo na kufariji, na ambavyo anasema anaendelea kuvisambaza katika shule mbalimbali, baadhi yavyo akivitoa bila malipo.

Vitabu hivyo alivyotunga kwa lugha ya Kiingereza, vinajumuisha: God is not done with you yet, Dark pasts brighter tomorrow na Redefining your life.

Ni mtunzi wa vitabu mbalimbali vya kufariji na mafunzo. PICHA/ SAMMY WAWERU

Vingine ni: The Three Pillars of A Believers’ Life, In The Mind of a New Believer pamoja na The Dawn of Salvation, ambapo kufikia sasa amesambaza zaidi ya nakala 5,000.

“Katika shule ya upili, nyakati zingine nililala njaa. Sikufa moyo kuafikia ndoto zangu. Ninalenga kuwapa moyo wanafunzi na vijana wanaopitia changamoto, Mungu ni mwaminifu, hatowaachilia,” anahimiza.

Nicholas Muturi anaungama ameshuhudia ufanisi maishani kupitia neema za Mwenyezi Mungu, kuanzia akiwa kinda hadi kukomaa kwake.

Aidha, anasema malengo yake ya mwaka ujao, 2021, ni kurejea chuo kikuu kuendeleza azma yake kukata kiku cha masomo.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo, alifichua kwamba atajiunga na Chuo Kikuu cha Mt Kenya, kusomea Shahada ya Elimu (Somo la Hisabati na Kemia).